Kizaramo ‘mibili’ kilivyozaa Muhimbili | Mwananchi

Nenda kokote Tanzania jina Muhimbili utalikuta sehemu moja tu, napo ni jijini Dar es Salaam.

Si kama Kariakoo, Magomeni, Mbuyuni, Majengo na majina mengine  kadhaa utakayoyakuta mikoa mbalimbali.

Jengo la iliyokuwa Hospitali ya Sewa Haji.

Lakini Muhimbili ya Dar si eneo pekee bali ni kile kilichopo hapo. Hapa ndipo ilipo hospitali kuu zaidi nchini.  Hii ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Inawezekana hujui chimbuko la hospitali hii. Makala haya yana msaada kwako. Historia inaonyesha mahala ilipo Hospitali ya Muhimbili awali miaka ya mwishoni mwa 18900, kulijengwa hospitali ndogo iliyoitwa Sewa Haji, ikibeba jina la msamaria mmoja aliyetoa mali yake kujenga kituo hicho akitwa Sewa Haji Paroo.

Sewa Haji  alikuwa  mfanyabiashara na tajiri mkubwa Tanganyika na Afrika Mashariki, ndiye  aliyeweka msingi wa majengo ambayo baadaye ikaja kuwa Hospitali ya Muhimbili. Aliacha wosia kuwa hospitali aliyoiasisi ije kuendeshwa na Serikali.

Kufika mwaka 1919 Serikali ya kikoloni ilikabidhiwa hospitali hiyo na ikawa inatumika kwa ajili ya wagonjwa wa Kiafrika.

Yalipoongezeka majengo miaka ya 1950, jina la Sewa Haji likabadilishwa na kuwa Dar es Salaam General Hospital  na baadaye  Princess Margaret Hospital.

Kilichotokea baada ya Uhuru

Baada ya Uhuru mwaka 1961, hospitali hiyo ilianza kujulikana kwa jina la Muhimbili.  Kwa nini  iliitwa Muhimbili? Wazaramo watatujibu swali hili.

Simulizi za kihistoria zinaeleza kuwa kwa kuwa hospitalini  ndipo watoto walipozaliwa,   wenyeji ambao ni Wazaramo walikuwa wakitumia neno ‘mibili’ yaani kondo la nyuma la mama baada ya kujifungua.

Walizoea kusema kuwa hapo ndipo kinamama walikuwa wakienda kuacha mibili yao.

Sewa Haji enzi za uhai wake. Ndiye anayetajwa kuasisi hospitali ya Sewa Haji ambayo baadaye ilikuja kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Matumizi makubwa ya neno mibili, hatimaye yakazaa neno Muhimbili, kwa mujibu wa simulizi za kihistoria.

Muhimbili sio hospitali pekee, lakini pia kuna Chuo Kikuu cha Sayansi za tiba maarufu kwa kifupi cha Muhas. Msingi wa chuo hiki ulianza mwaka 1963 kilipoanzishwa kwa jina la Chuo cha Afya Dar es Salaam.

Aidha, kumuenzi  msamaria mwema  na muungwana huyu aliyeweka msingi wa hospitali hiyo kongwe nchini, Muhimbili ya sasa ina wodi maalum inayoitwa Sewa Haji.

Sewa Haji hakumbukwi kwa kuweka msingi Hospitali ya Muhimbili pekee, anatajwa kama miongoni mwa matajiri waliotumia mali zao kusaidia wanyonge katika historia ya Tanganyika.

Hakubagua nani wa kumsaidia, kwake yeyote aliye na uhitaji awe na asili ya Afrika au nje alipata nafasi ya ukarimu wake.

Alikuwa mchamungu na tajiri aliyeshangaza wengi kwa kuwa karibu na wapagazi kiasi cha kufikia hatua ya kukla pamoja nao, jambo ambalo halikuwa limezoeleka enzi hizo za wapagazi walioonekana kuwa kama nusu watu.

Licha ya mafungamano yake na dini ya Kiislam kupitia madhehebu ya Ismailia, bado Sewa Haji alikuwa karibu na madhehebu mengine hasa Kanisa Katoliki mjini Unguja analotaja kuwahi kulifadhili kiasi cha kufikia kumwita mja na rafiki mwema.

Mwaka 1892 alijenga jengo la ghorofa tatu mjini Bagamoyo na likatumika kaka shule inayopokea watoto mchanganyiko.

Aidha aliwahi kuanzisha nyumba ya kuishi wapagazi na watu wenye ukoma.

Alifariki mwaka 1897 akiwa na miaka 46 na kuacha huzuni kubwa kwa wakazi wa Bagamoyo.

Related Posts