Ubunifu ulivyofaulisha wanafunzi darasa la saba

Dar es Salaam. Kuna msemo wa Kiswahili usemao ‘kitu ukikipenda utakifanya kwa moyo na kutamani kupata matokeo chanya katika kile unachokifanya.’

Bila kujali matokeo yatachukua muda gani, lakini utaweka nia huku ukiongeza ubunifu, uvumbuzi ili kuhakikisha malengo yako yanafikiwa.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa mwalimu Yusuph Pangoma, ambaye sasa anajivunia wanafunzi wake kupata matokeo mazuri ya darasa la saba, huku akikumbuka safari yao ya miaka sita tangu alipowapokea wakiwa darasa la pili. Wanafunzi watano kati yao ndiyo walikuwa wakijua kusoma na kuandika.

Pangoma anayefundisha Shule ya Msingi Ikorongo iliyopo mkoani Mara ambayo katika matokeo hayo wanafunzi 10 pekee kati ya 117 ndiyo waliopata daraja D, huku kukiwa hakuna daraja E na saba wakipata wastani wa alama A.

“Wanafunzi hawa niliwapokea mwaka 2019 wakiingia darasa la pili wakiwa hawajui kusoma na kuandika isipokuwa watano pekee, wakati huo ndiyo nilikuwa mgeni katika ajira, hivyo nikaweka malengo kuhakikisha wanafaulu masomo yao ya kumaliza elimu msingi,” amesema Pangoma alipozungumza na Mwananchi juzi, Novemba 2, 2024.

Pangoma ambaye ni mwalimu maarufu katika mtandao wa kijamii wa Instagram kutokana na mbinu zake za ufundishaji anazotumia, amesema hali hiyo ilimfanya kuanza kubuni mbinu mbalimbali za kufundishia, ikiwemo nyimbo, sarakasi, zana mbalimbali za kufundishia, kujenga urafiki na wanafunzi ili kuwaondolea hofu waliyokuwa nayo.

“Jitihada hizi sikuzifanya peke yangu, tulishirikiana na walimu wengine tuliokuwa tumeingia wote katika ajira kwa wakati huo, jambo la kwanza lilikuwa ni kurudisha ari ya wanafunzi na kuwaongezea hamasa ya shule, licha ya mazingira wanayotoka,” amesema Pangoma.

Amesema njia nyingine iliyokuwa ikiongeza ushindani kwa wanafunzi hao ni kutolewa zawadi kwa wanafunzi waliokuwa wakifanya vizuri katika mitihani mbalimbali, ikiwemo kuwachinjia kuku, kuwanunulia soda.

“Pia kuwanunulia mavazi kama nguo ili hata waliokata tamaa wapate moyo wa kusoma na wafaulu, kwetu ni matokeo makubwa. Hii imefanya hata shule yetu kuwa ya kwanza katika ukanda wa Ngoreme wenye shule 17 na imefanikiwa kutoa wanafunzi watakaokwenda shule za vipaji maalumu,” amesema Pangoma.

Kwa mara ya kwanza Mwalimu Pangoma alifanya mazungumzo na Mwananchi mwaka 2023 huku akielezea mbinu zake za ufundishaji anazotumia na namna ambavyo zimekuwa zikihamasisha na kurahisisha ujifunzaji wa watoto.

Mbali na kuwa mwalimu, Pangoma pia amekuwa akitumia mtandao wa kijamii wa Instagram katika kuhamasisha wafuatiliaji wake (follower) kutoa michango ya vitu mbalimbali, ikiwemo nguo, viatu, madaftari na vifaa vingine vya kujifunzia kwa wanafunzi wake.

Hiyo ni kwa sababu, wanafunzi wengi wa shule anayofundisha wanatoka katika familia duni, jambo linalofanya baadhi kwenda shuleni wakiwa hawana viatu, nguo zilizochanika au madaftari yaliyojikunja, jambo linalowanyima uhuru wa kujifunza.

Mwalimu huyu amekwenda mbali na sasa amekuwa msaada katika jamii inayomzunguka hasa baada ya kuanza kutumia ukurasa wake huo wa Instagram kuwaombea wakazi mbalimbali wa kijiji chake misaada, ikiwemo ya fedha kwa ajili ya matibabu kwa watu hata wasiokuwa wanafunzi, shughuli za kiuchumi hata kuboresha makazi ya baadhi ya wanafunzi.

Pangoma ambaye ni mzaliwa wa Jiji la Dar es Salaam, alimaliza kidato cha nne mwaka 2009 katika Shule ya Sekondari Tandika na kupata ufaulu wa daraja la tatu ambao ungemuwezesha kujiunga kidato cha tano, lakini alishindwa kumudu gharama za kujisomesha, kwani wazazi wake walikuwa wameshafariki.

Hali hiyo ilimfanya kuanza kujitolea kufundisha vijana wa kidato cha pili na kwanza katika maeneo tofauti na baadaye aliona kazi ya ualimu inanifaa na anaipenda, ndipo aliamua kujiunga na chuo cha ualimu Ilonga Morogoro.

Alimaliza chuo mwaka 2015, alitoka na lengo moja la kufanya mageuzi katika ufundishaji, lakini alijikuta akikaa mtaani bila ajira kwa muda kabla ya kupangiwa kituo cha kazi mwaka 2018 wilayani Serengeti.

Mbali na kuwa mwalimu, Pangoma amesema katika miaka mitano ijayo anajiona akitumiwa na taasisi mbalimbali kama mwezeshaji kuwashawishi walimu kutumia mbinu zake za ufundishaji, ili waweze kufundisha watoto kwa upendo.

Pia kuwa mwezeshaji wa taifa kuwezesha wafanyakazi, walimu, kuwafundisha walimu namna ya kujishusha katika kazi, kubeba tabia za wanafunzi katika ufundishaji.

Anasema katika kipindi hicho anatamani kuwa na taasisi itakayosaidia watoto kupata mahitaji muhimu ya shule, ikiwemo sare ili waweze kujifunza vizuri.

Related Posts