Kamisheni ya uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), imesema uchaguzi wa Kamati hiyo msimu huu utafanyika Desemba 14 mjini Dodoma.
Nafasi 12 zitawania huku ile ya katibu mkuu inayoshikiliwa na mwanariadha wa zamani, Filbert Bayi ikiondolewa kwenye zile zinazopigiwa kura baada ya katiba kufanyiwa mabadiliko na sasa itakuwa ya kuajiriwa.
Nafasi nyingine itakayokuwa ya kuajiriwa ni ya mweka hazina.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya uchaguzi huo, Ibrahim Mkwawa amesema nafasi zinazowaniwa sasa ni ya rais na makamu wa rais, sanjari na wajumbe 10, nusu kutoka Bara na nusu kutoka Zanzibar.
“Hawa wajumbe watano watano watakaochaguliwa, wawili wanapaswa kuwa wanawake kila upande, yaani Bara na Visiwani,” alisema Mkwawa
Alisema fomu za kugombea zimeanza kutolewa jana Jumanne hadi Novemba 11,2024 makao makuu ya TOC, Dar es Salaam na kwenye ofisi za Chama cha Diabetics visiwani Zanzibar.
“Kama Kamisheni, kazi yetu ni kuandaa, kusimamia na kutangaza matokea ya uchaguzi huu kwa mujibu wa Katiba ya TOC na kanuni za uchaguzi,” amesema.
Akitaja sifa za wagombea, Mkwawa amesema kwanza lazima wawe Mtanzania, mwenye akili timamu, awe na uzoefu olimpiki, awe na elimu ya kuanzia sekondari, awe na uzoefu wa masuala ya utawala wa michezo kitaifa na kimataifa.
“Pia asiwe ameshtakiwa katika kosa
la jinai, awe anawakilisha vyama vya michezo vinavyotambuliwa na TOC na awe amehudhulia mafunzo na semina za michezo.
“Kuna sifa za ziada kwa watakaogombea uraia na makamu wa rais, hawa lazima awe na digrii ya chuo Kikuu awe na uwezo wa kuiwakilisha TOC kitaifa na kimataifa na asiwe amefukuzwa au kuzuiwa kugombea kwenye vyama vilivyo chini ya TOC na gharama ya fomu ya nafasi hizo ni Sh 500,000 huku za wajumbe ni Sh 200,000.
Awali, Katibu mkuu anayemaliza muda wake, Filbert Bayi alisema uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) unazitaka nchi wanachama kufanya chaguzi ndani ya miezi sita baada ya michezo ya Olimpiki.
“Viongozi wapya watakaochaguliwa watahudumu madarakani kuanzia 2025-2028,” alisema Bayi.
Alisema uchaguzi mkuu wa TOC utatanguliwa na ule wa Kamisheni ya wanamichezo, Desemba 8, kisha wa Olimpians Desemba 10 ba kufuatiwa na semina ya Makatibu Wakuu wa Vyama vya Michezo vilivyo chini ya TOC, Desemba 12 mkoani Dodoma.