Dar es Salaam. Mshitakiwa Felista Mwanri (70) na wenzake watano wanaokabiliwa na shitaka la kusafirisha tani moja ya dawa za kulevya aina ya bangi wanaendelea kushikiliwa rumande kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.
Wakili wa Serikali, Rhoida Mwakamele leo Novemba 5, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini amedai upelelezi unaendelea, hivyo ameiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa.
Hakimu Mhini amekubali ombi hilo la upande wa mashitaka na kuahirisha kesi hadi Novemba 19, 2024 kwa ajili ya kutajwa.
Washitakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shitaka linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.
Mbali ya Mwanri mkazi wa Luguruni, washitakiwa wengine ni mtoto wake Richard Mwanri (47), Athuman Mohamed maarufu Makame (58) mkazi wa Tanga, Juma Chappa (36) mkazi wa Kiwalani, na Omary Mohamed (32), dereva na mkazi wa Buza, Dar es Salaam.
Washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 28, 2024 eneo la Tairo, Luguruni barabara ya Kwembe ndani ya Wilaya ya Ubungo.
Wanadaiwa siku ya tukio walikutwa wakisafirisha bangi yenye uzito wa kilo 1,815 kinyume cha sheria.
Kwa mara ya kwanza washitakiwa walifikishwa mahakamani hapo, Septemba 10, 2024 na kusomewa shitaka hilo.
Shauri hilo limesikilizwa kwa njia ya video washitakiwa wakiwa rumande.