Wakati idadi ya makocha wanaoomba kibarua Ken Gold ikizidi kuongezeka, uongozi wa timu hiyo umesema mbali na vigezo vya elimu, unataka kocha mwenye historia ya matokeo mazuri.
Ken Gold ya wilayani Chunya mkoani Mbeya inatarajia kushiriki Ligi Kuu msimu ujao baada ya kupanda daraja na kumaliza Championship ikiwa kinara kwa pointi 70 ikifuatiwa na Pamba Jiji iliyovuna alama 67.
Taarifa ilizopata Mwanaspoti ni kuwa zaidi ya makocha wanane kutoka mataifa tofauti ikiwamo Tanzania, Congo na Ufaransa tayari wamewasilisha maombi kufanya kazi kwa wachimba dhahabu hao.
Timu hiyo inahitaji kocha mkuu kufuatia aliyeipandisha Jumanne Challe kutokidhi vigezo kwa kuwa na leseni B ya Caf, hivyo kufanya uongozi kusaka mtu mpya.
Mkurugenzi wa timu hiyo, Keneth Mwambungu aliliambia Mwanaspoti kuwa hawataangalia majina ya mtu wala utaifa wake, bali historia ya mafanikio alipowahi kufanya kazi.
Alisema kutokana na malengo waliyonayo msimu ujao, hawatakurupuka kuajiri kocha kwa kuangalia sura yake, isipokuwa wanahitaji mtu sahihi mwenye uwezo na ushirikiano.
“Tunataka kocha mkuu ambaye ana historia yake kimafanikio, siyo kuangalia uraia wake au sura, tunayo malengo yetu na hatutakurupuka kwa namna yoyote,” alisema Mwambungu.
Kigogo huyo aliongeza kuwa wanahitaji kuanza maandalizi ya mapema.