Dar es Salaam. Msanii wa muziki, Ferdnand Ndikuriyo (27) maarufu kama Chuma wa Chuma, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa, kujibu shtaka moja la kuwepo nchini bila kuwa na kibali.
Chuma ambaye ni raia wa Burundi na mkazi wa Mbezi Louis, amefikishwa Mahakama hapo leo Jumanne, Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya jinai namba 31005/2024 na Wakili wa Serikali, Ezekiel Kibona akishirikia na Mohamed Mlumba, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.
Kibona amedai kuwa, Chuma alitenda kosa hilo Septemba 18, 2024 eneo la Las Vegas Casino, lililopo Upanga, Wilaya ya Ilala.
Inadaiwa kuwa, mshitakiwa akiwa eneo hilo, alibainika kuwepo nchini bila kuwa na kibali, wakati akijua ni kosa kisheria.
Mshitakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo, alikana na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo waliiomba Mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Pia, Serikali imewasilisha pingamizi la kuzuia dhamana ya mshitakiwa huyo kutokana na sababu za kiusalama.
“Mheshimiwa hakimu, tumewasilisha ombi la kuzuia dhamana dhidi ya mshitakiwa huyo kutokana na sababu za kiusalama,” amedai Kibona.
Hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 6, 2024 kwa ajili ya kusikiliza maombi hayo na mshitakiwa amerudishwa rumande hadi kesho.