Vigogo waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali kwenye timu za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti wametangazwa na Singida Black Stars kushika nyadhifa mbalimbali kwenye klabu hiyo.
Viongozi hao waliowahi kuongoza Yanga na sasa wako Singida ni pamoja na Omary Kaya ambaye ameteuliwa kuwa makamu mwenyekiti.
Kabla ya kujiunga na Singida Black Stars, Kaya alikuwa mtendaji mkuu wa Namungo na aliwahi kukaimu nafasi ya ukatibu mkuu Yanga.
Mwenyekiti wa zamani wa kamati ya usajili ya Yanga, Hussein Nyika ameteuliwa kuwa mjumbe wa bodi kama ilivyo kwa Fatema Dewji ambaye ni dada wa Rais wa heshima wa Simba, Mohamed Dewji MO.
Ikumbukwe kwamba Fatema ndiye mlezi wa timu ya wanawake ya Simba, Simba Queens.
Yupo pia mbunge wa Makete, Festo Sanga ambaye ni shabiki wa Simba aliyepata ujumbe.
Vilevile aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Dk Athuman Kihamia ni miongoni mwa wajumbe walioteuliwa kuunda bodi hiyo.
Viongozi waliotangazwa kuunda bodi ya klabu hiyo ni Ibrahim Mirambo (mwenyekiti wa bod)i, Kaya (makamu mwenyekiti), Jonathan Kassano ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa timu hiyo.
Wengine waliotangazwa na klabu hiyo ni pamoja na ni Sanga (mjumbe) Wiltrudie Mutembei (mjumbe) Seif Ahmes (mjumbe) Nickson Malick (mjumbe), Nyika (mjumbe) Samm Madelu (mjumbe), Dk Kihamia (mjumbe),
Fatema (mjumbe ) pamoja na Salah Mohamed (mjumbe).
Singida Black Stars ya mkoani Singida imeanza msimu huu ikiwa na matokeo mazuri ambapo tangu ibadilishwe jina kutoka Ihefu na kuwa Singida Black Stars imekuwa moto wa kuotea mbali.
Katika michezo 10 iliycheza kwenye Ligi Kuu Bara imekusanya alama 22, ikiwa imefunga mabao 13 na kuiruhusu manne ambapo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.