Mauya: Ni msimu wa akili, mbinu

WAKATI kukiwa na ushindani mkubwa katika Ligi Kuu Bara msimu huu, kiungo wa Singida Black Stars, Zawadi Mauya amesema ili timu ipate matokeo mazuri nyumbani na ugenini, inahitajika wachezaji kutumia mbinu, akili na kucheza kwa kiwango cha juu muda wote.

Kiungo huyo aliifafanua kauli yake akiitolea mfano Yanga ilivyokuwa inafunga mabao mengi msimu uliopita na ilivyouanza huu kwa idadi ndogo ya mabao.

Mauya ambaye msimu uliopita alikuwa na kikosi cha Yanga, alishuhudia timu yake ikitoa vipigo vikubwa ndani ya ligi ikiwemo ushindi wa 5-0 dhidi ya KMC na JKT Tanzania na pia 5-1 mbele ya Simba.

“Kwa matokeo ambayo zimepata timu mbalimbali za Ligi Kuu hadi sasa yanatafsiri namna msimu ulivyo na ushindani mkali. Inahitajika mbinu na akili kubwa ili kushinda mechi siyo, nyumbani wala ugenini, kwani hakuna timu ambayo imekaa kinyonge.

“Simba na Yanga zinashinda bao moja ama mawili, tofauti na msimu uliopita hata ukiangalia washambuliaji wana kazi ya kufanya ili kumiliki mabao mengi,” alisema Mauya.

Kiungo huyo ambaye msimu huu amejiunga na Singida Black Stars, amesema wana benchi la ufundi imara na uongozi bora kitu kinachochangia kutoa ushindani mkali dhidi ya timu pinzani.

“Ukiangalia benchi la ufundi utagundua linafanya kitu kikubwa, tumeanza vizuri katika mzunguko wa kwanza, tunatamani kuendelea na mapambano hayo ili uwe msimu wa kihistoria kwetu,” alisema Mauya na kufafanua sababu ya kutoonekana uwanjani mara kwa mara.

“Kuhusu kutoonekana kucheza mechi mara kwa mara. Nilikuwa nauguza majeraha, sikuanza na timu wakati inafanya maandalizi ya msimu kwa sasa ndio nimerudi najitafuta, lakini wanaocheza nafasi yangu wapo vizuri sana.”

Singida Black Stars inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 10 na kukusanya pointi 23 ikishinda saba, sare mbili na kupoteza moja.

Related Posts