VIDEO: RC Chacha apiga marufuku uuzaji majeneza nje ya hospitali

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amemuagiza katibu tawala wa mkoa huo kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanya biashara wa majeneza ili waondoe shughuli zao nje ya Hospitali ya Kitete.

Amesema kuendelea kufanya biashara hiyo  maeneo hayo tena hadharani, kunatajwa kuongeza hofu kwa wagonjwa wanaopelekwa kupata matibabu pindi wayaonapo yamepangwa nje.

Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 5, 2024 baada ya kutembelea hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora na kushuhudia wafanya biashara wa majeneza wakifanya shughuli zao mbele ya lango kuu la hospitali hiyo.

Chacha amesema kuna baadhi ya wagonjwa wanaweza kukata tamaa na kuingiwa na hofu baada tu ya kuona jeneza mbele yake.

“Wakati tunaingia hapa tumeona majeneza yanachongewa mbele ya geti kuu ambalo wagonjwa wanalitumia kuingilia, tunajua sote ipo siku moja tutakufa, lakini sio jambo jema mgonjwa anakuja kutibiwa anakutana na jeneza kabla hata hajamuona daktari, nimemuelekeza Katibu tawala kwa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri wote mkoani hapa, watenge maeneo maalumu kwa watoa huduma hii,” amesema Chacha.


Majeneza kuuzwa karibu na hospitali yaibua mpya

Amesema hawatawafukuza kwa sasa, ila wanawapatia muda wa miezi mitatu na baada ya hapo watapatiwa eneo maalumu la kujenga mabanda ya kuuzia maeneza hayo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, DK John Mboya amesema maelekezo yaliyotolewa na mkuu wa mkoa huo, yatafanyiwa kazi.

Akizungumzia kauli hiyo ya mkuu wa moa, mfanyabiashara wa majeneza eneo la Hospitli ya Kitete, Essau Clemence amesema;

“Ni kweli wapo baadhi ya wagonjwa huingiwa na hofu, ila kwa upande wetu hatukuwa tunaona kama kuna shida, ila tutazingatia alichosema.”

Mkazi wa Manispaa ya Tabora, Lucas Masanja amesema aliwahi kupata ajali akapelekwa hospitlini hapo akiwa na hali mbaya, alipofika getini akitazama kushoto na kulia kote anaona majeneza, alihisi ndiyo mwisho wa maisha yake.

Naye Halima Ikunji, mkazi wa Ipuli Manispaa ya Tabora amesema wagonjwa wengine wanaogopa kufanya mazoezi kwa kuhofia kuyaona majeneza.

Mtaalamu wa afya ya akili atoa neno

Mtaalamu wa afya ya akili, Swaum Kimaro amekiri kuwa wapo baadhi ya wagonjwa n ahata wanaowauguza hupatwa na hofu baada ya kuona majeneza.

“Wagonjwa wanaopata hofu wengi wao ni wale wenye shinikizo la damu na wengi wao wanakuwa na wasiwasi na mara nyingi wakiona majeneza wakitafakari ugonjwa wao, hofu inajengeka kwa kiasi kikubwa na inaweza kusababisha matatizo kwao,” amesema Kimaro.

Hata hivyo, amesema watu wanapaswa kupata ushauri nasihi kwamba kila mtu ipo siku ataonja mauti, hivyo hakuna haja ya kuwa na hofu.

Related Posts