Wadau wahimizwa kujitokeza kutoa elimu ya uzalishaji mbegu bora za mpunga kwa wakulima

-Lengo ni kuongeza uzalishaji

Na Esther Mnyika, Pwani

Wadau wa masuala ya kilimo wametakiwa kujitokeza kutoa elimu ya uzalishaji mbegu bora kwa wakulima wa mpunga ili kutatua changamoto ya upungufu wa mbegu nchini na kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga. Wito huu ulitolewa Novemba 4, 2024, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya uzalishaji wa mbegu za ubora za mpunga (UKU), yaliyofanyika wilayani Bagamoyo.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga (IRRI) na kuvikutanisha vikundi mbalimbali vya uzalishaji mbegu kutoka mikoa tofauti nchini.

Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo Wilaya ya Bagamoyo, Gerald Mwamuhamila, alisema kuwa ni muhimu sasa kwa wadau kujitokeza kwa wingi ili kutoa elimu kwa wakulima kuhusu uzalishaji wa mbegu bora za mpunga. Alisisitiza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kutatua changamoto ya upungufu wa mbegu za mpunga, hali ambayo imekuwa ikiwakabili wakulima wengi nchini.

“Lengo la mafunzo haya ni kuzalisha mbegu za kuazimia ubora, na kufanya hivyo kutasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa mbegu za mpunga ambazo zinawakabili wakulima. Wakulima hawa watakuwa na jukumu la kuzalisha mbegu bora pindi watakapomaliza mafunzo haya,” alisema Mwamuhamila.

Mwamuhamila alifafanua kuwa wakati mwingine wakulima wengi wanatumia mbegu za mpunga zinazojirudia, jambo linalosababisha uzalishaji mdogo. Aliweka wazi kwamba katika baadhi ya maeneo, kama vile kikundi cha uzalishaji mbegu cha Bagamoyo, wakulima wanazalisha tani mbili na nusu tu kwa hekta moja, wakati uzalishaji wa mpunga wa kutosha kwa kutumia mbegu bora unapaswa kuwa tani nne kwa hekta moja.

“Kupitia mafunzo haya, tunatarajia kufikia lengo la uzalishaji wa tani sita kwa hekta moja ifikapo mwaka 2030,” aliongeza Mwamuhamila.

Mafunzo hayo yalihusisha washiriki 35 kutoka vikundi 13 vya uzalishaji wa mbegu kutoka wilayani Bagamoyo pamoja na wawakilishi wa vikundi kutoka mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Katavi, Mbeya na mingineyo. Baada ya mafunzo, washiriki wanatarajiwa kuzalisha mbegu zitakazothibitishwa na Wakala wa Mbegu Nchini (ASA) na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Nchini (TOSCI).

Afisa Miradi wa Shirika la Maendeleo ya Kilimo Afrika Mashariki (EACD), Robert Mwalubeke, alieleza kuwa mafunzo hayo yanakusudia kuongeza upatikanaji wa mbegu bora nchini, kwani bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa mbegu za mpunga.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya wakulima nchini bado wanategemea mbegu zilizozalishwa mara nyingi, jambo linalosababisha mavuno madogo na ubora mdogo wa mpunga.

“Zaidi ya wakulima asilimia 70 wanarudia mbegu, huku chini ya asilimia 30 wakipanda mbegu mpya. Hii ni fursa muhimu, kwani kurudia mbegu kunaathiri mavuno, ubora wa mpunga, na hatimaye kipato cha mkulima,” alisema Mwalubeke.

Neema Japhet, mshiriki kutoka kikundi cha Tuinuane Kiuchumi cha mkoa wa Rukwa, alisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuboresha kilimo cha mpunga katika mkoa wao. Alisema kuwa wanatarajia kutumia elimu hiyo kuwasaidia wakulima wakiwa na mbegu bora, ili kuongeza uzalishaji na kuondoa upungufu wa mbegu katika mkoa wao.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima nchini, kwani yatawasaidia kupata mbegu bora kwa wakati na hivyo kuongeza uzalishaji wa mpunga, kuboresha kipato cha wakulima, na pia kusaidia katika kutatua changamoto ya uhaba wa chakula.

Related Posts

en English sw Swahili