Kura za uchaguzi wa urais Marekani zaendelea kuhesabiwa – DW – 06.11.2024

Kinyang’anyiro cha kuingia katika Ikulu ya White House kati ya mgombea wa chama cha Republican Donald Trump na mgombea wa chama cha Democratic Kamala Harris kinaonekana kuwa kikali, huku taifa hilo likisubiri kwa hamu matokeo ya mojawapo ya uchaguzi mkali zaidikatika historia ya Marekani

Matokeo ya uchaguzi huo yataamua iwapo yatamuweka madarakani Harris na kuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya kuliongoza taifa hilo lenye nguvu duniani, au kumrejesha Trump madarakani.

Majimbo yaliyotangazwa 

Matokeo ya awali yanaonesha kuwa mgombea wa chama cha Republican Donald Trump amepata kura 198 za wajumbe wa kamati maalum ya uchaguzi nchini Marekani, ambayo inamchagua Rais maarufu kama Electoral College, na mgombea wa chama cha Democratic, Kamala Harris amepata kura 109 za Electoral College.

Trump ameshinda katika majimbo ya Kentucky, Indiana, West Virginia, Florida, Oklahoma, Tennessee, Alabama, South Carolina, Wyoming, South Dakota, Texas, Arkansas, Ohio na Nebraska.

Mgombea wa chama cha Democratic, Kamala Harris
Mgombea wa chama cha Democratic, Kamala Harris Picha: Andrew Harnik/Getty Images

Huku Harris akishinda kwenye majimbo ya Vermont, Maryland, Connecticut, New England, Rhode Island, New York na Delaware, ambako ni nyumbani kwa Rais Joe Biden.

Majimbo mengine aliyoshinda Harris ni Mississippi, Massachusetts, New Jersey, Illinois, ambako ni nyumbani kwa rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama. Jimbo hilo limekuwa likiwachagua wagombea wa Democratic tangu mwaka 1992.

Ushindi wa Trump Florida, ni wa mara ya tatu mfululizo. Mgombea wa urais wa chama cha Democratic hajawahi kushinda kwenye jimbo hilo, tangu Barack Obama aliposhinda mwaka 2012.

Mshindi anahitaji kupata kura 270

Kila mgombea anahitaji kupata kura 270 za Electoral College kati ya 538 zinazohitajika ili kushinda.

Katika matokeo ya kura za wananchi wa kawaida zilizohesabiwa hadi muda huu tunakwenda hewani, Harris kapata kura milioni 21,199,192 ambazo ni sawa na asilimia 46.3, na Trump kura milioni 24,234,518 ambazo ni sawa na asilimia 52.6.

Katika uchaguzi wa maseneta, chama cha Republican kimepata 46 na Democratic 35. Aidha, chama cha Republican kimepata wabunge 73 na Democratic wabunge 40, na kwa upande wa magavana, Republican imepata 23 na Democratic 22.

Mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump
Mgombea wa chama cha Republican, Donald TrumpPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Matokeo ya urais wa Marekani yanaweza kujulikana punde tu baada ya siku ya uchaguzi, au yanaweza kuchukua wiki kadhaa hadi yatakapothibitishwa.

Akizungumza kabla ya vituo vya kupiga kura kufungwa, Trump aliwatolea wito wafuasi wa Republican kuhakikisha wanapiga kura zao, akiwataka walioko katika foleni waendelee kusubiri hadi watakapopiga kura.

Kwa upande wake Harris alikuwa akiwapigia simu wafuasi wake kuwashukuru kwa kujitokeza kwao kupiga kura.

Urusi yakanusha madai ya kuingilia uchaguzi wa Marekani

Huku hayo yakijiri, kuliripotiwa kitisho cha mabomu kwenye vituo vya kupigia kura huko Georgia. Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI na polisi wa eneo hilo wamesema kulikuwepo taarifa za vitisho 32 vya mabomu vinavyoonekana kutokea Urusi, ambayo imeshutumiwa na Marekani kwa kujaribu kuuingilia uchaguzi wa urais.

Kitisho hicho kilisababisha kufungwa kwa muda kwa vituo vitano vya kupigia kura, ili kuwaruhusu polisi kufanya uchunguzi wa vilipuzi hivyo, ingawa hawakukuta kitu chochote.

Hata hivyo, ubalozi wa Urusi nchini Marekani umekanusha madai kwamba nchi hiyo imeuingilia uchaguzi wa urais nchini Marekani na kuyaita madai hayo kuwa ni ”kashfa ya uwongo”.

Nani kuibuka mshindi?

Harris kuchuana vikali na Trump. Nani kuibuka mshindi leo?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

 

(AFP, DPA, AP, Reuters)

Related Posts