Tel aviv. Maandamano yamezuka nchini Israel, baada ya Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu kumfuta kazi Waziri wa Ulinzi, Yoav Gallant.
Hatua ya kumfuta kazi waziri huyo inatokana na kile kinachodaiwa hakukuwa na uaminifu kati yake na Gallant.
Netanyahu amesema imani yake kwa Gallant imepungua katika miezi ya hivi karibuni, huku akimchagua Waziri wa Mambo ya Nje, Katz kuchukua nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa BBC, Gallant amesema kuondolewa kwake kumetokana na kutokubaliana katika masuala matatu, ikiwa ni pamoja na imani yake kwamba inawezekana kuwarejesha mateka waliosalia kutoka Gaza.
Hata hivyo, inaelezwa Netanyahu na Gallant kwa muda mrefu wamekuwa na mgawanyiko kuhusu mkakati wa vita wa Israel.
Miezi kadhaa kabla ya kuanza kwa vita huko Gaza Oktoba 2023, Netanyahu alimfukuza Gallant kutokana na tofauti za kisiasa, kabla ya kumrejesha kazini baada ya malalamiko makubwa ya umma.
Kutokana na hatua hiyo, baada ya kupata taarifa waandamanaji wameibuka mitaani katika kituo cha kibiashara cha Israel Tel Aviv, wakifunga barabara kuu ya mji huo na kuwasha moto.
Mamia ya waandamanaji wamekusanyika mbele ya makazi ya Netanyahu mjini Jerusalem. Waandamanaji pia walifunga barabara katika maeneo mengine.