Kipa wa Simba, Moussa Camara ni miongoni mwa wachezaji 23 walioitwa katika kikosi cha Guinea kitakachocheza mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 dhidi ya DR Congo na Tanzania ‘Taifa Stars’ baadaye mwezi huu.
Guinea itakuwa nyumbani, Novemba 16 kuikabili DR Congo na baada ya hapo, Novemba 19 itakuwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kukabiliana na Taifa Stars.
Camara ndiye alidaka mechi mbili zilizopita za Guinea za mashindano hayo ya kuwania kufuzu dhidi ya Ethiopia ambazo zote ilipata ushindi.
Kocha wa Guinea, Michael Dussuyer amemjumuisha beki wa Kayserispor ya Uturuki, Julien Janvier ambaye hakucheza mechi zote nne zilizopita za kuwania kufuzu Afcon 2025 ambazo Guinea ilipata ushindi katika mechi mbili na kupoteza mbili.
Janvier anachukua nafasi ya Mohamed Ali Camara ambaye safari hii hajajumuishwa kikosini kwa ajili ya mechi hizo muhimu kwao.
Kikosi hicho cha Guinea kimesheheni nyota wanaocheza soka la kulipwa katika klabu mbalimbali barani Ulaya wakiongozwa na mshambualiaji wa Borussia Dortmund, Serhou Guirassy.
Guirassy ambaye alikosa mechi mbili za mwanzo za kufuzu za Guinea dhidi ya DR Congo na Tanzania, ndiye kinara wa kufumania nyavu katika mashindano hayo ya kuwania kufuzu Afcon 2025 akiwa na mabao matano.
Wachezaji 23 wanaounda kikosi cha Guinea ni makipa Moussa Camara, Kemo Touré na Mory Keita huku mabeki wakiwa ni Julien Jeanvier, Antoine Conte, Ibrahim Sory Conte, Ibrahim Diakité, Naby Oulare, Saïdou Sow, Issiaga Sylla na Sekou Oumar Sylla.
Viungo walioitwa ni Aguibou Camara, Seydouba Cissé, Cheick Oumar Conde, Morlaye Sylla na Abdoulaye Toure na washambuliaji ni Aliou Badara Baldé, Algassime Bah, Mohamed Bayo, Kandet Diawara, François Kamano, Serhou Guirassy.
Guinea inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi H ikiwa imekusanya pointi sita huku kinara ikiwa ni DR Congo yenye pointi 12 wakati huo Taifa Stars inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne na inayoshika mkia ni Ethiopia yenye pointi moja.