WAZIRI KOMBO ATEMBELEA MAKUMBUSHO NCHINI CUBA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ametembelea makumbusho iliyohifadhi historia ya Muasisi wa Taifa la Cuba Komredi Fidel Castrol Ruz iliyopo jijini Havana, Cuba.

Waziri Kombo aliambatana na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na sehemu ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania uliopo nchini Cuba kushiriki Kongamano la Kimataifa la Kiswahili litakalofanyika tarehe 8 Novemba, 2024 jijini Havana.

Ziara hiyo imewezesha kufahamu masuala mbalimbali yaliyohifadhiwa katika makumbusho hiyo ikiwemo maisha aliyopenda kuyaishi, mavazi aliyokuwa akivaa kama vazi la jeshi, nguo ya mazoezi na michezo, pia kumbukumbu ya hotuba mbalimbali alizowahi hutubia ikiwemo Umoja wa Mataifa na kumbukumbu za shughuli mbalimbali alizofanya na viongozi wa Nchi za Afrika hususan wakati wa harakati za ukombozi wa Bara hilo.

Kwenye makumbusho hiyo pia kuna kumbukumbu za ziara za viongozi wa Tanzania waliotembelea nchini Cuba na ziara ya Komredi Fidel Castrol nchini Tanzania

Katika nafasi nyingine Waziri Kombo pia alitembelea Makumbusho iliyohifadhi historia ya nchi za kiafrika ambazo zimekuwa zikishirikiana kwa karibu na Cuba.

Makumbusho hiyo imehifadhi tamaduni mbalimbali za Afrika, inafundisha watoto tamaduni mbalimbali sambamba na lugha ambapo hivi karibuni inategemea kuingia makubaliano na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania ili kufundisha somo la Kiswahili. Vilevile, makumbusho hiyo imehifadhi kazi za sanaa zilizotengenezwa kwa chuma, mbao, gunia, kanga, kitenge n.k.







Related Posts