Dar es Salaam. Katika msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Bara, washambuliaji wa kati wa timu kubwa za Simba, Yanga, na Azam bado wanakabiliwa na changamoto ya kufumania nyavu.
Hadi kufikia mzunguko wa 11 wa ligi kwa baadhi ya timu, mastraika wa timu hizo maarufu wanaonekana kusota kupata mabao, hali ambayo imezua maswali na wasiwasi miongoni mwa mashabiki wa timu hizo licha ya kupata matokeo mazuri.
Katika msimu uliopita, washambuliaji wa timu hizo walikuwa na kasi ya juu ikilinganishwa na msimu huu. Kwa mfano, kipindi kama hiki mwaka jana, Simba walikuwa na mfungaji aliyekuwa na mabao tisa, Jean Baleke, ambaye kwa sasa amehamia Yanga na ana bao moja tu. Lakini msimu huu, hakuna mshambuliaji wa kati wa timu kubwa ambaye amefikisha idadi hiyo ya mabao ndani ya michezo 11.
Washambuliaji wa kati wa Simba, ambao ni Valentino Mashaka, Leonel Ateba na Steve Mukwala, kila mmoja ana mabao mawili tu hadi sasa.
Mabao haya mawili kwa kila mshambuliaji yanaonekana kuwa chini ikilinganishwa na matarajio ya timu na mashabiki wao.
Simba ilikuwa na matarajio makubwa kwa wachezaji hawa, hasa Mukwala ambaye alionyesha kiwango kizuri msimu uliopita akiwa na Asante Kotoko ya Ghana ambako alishika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora akiwa na mabao 14 nyuma kwa mabao matano aliyoachwa na Stephen Amankonah wa Berekum Chelsea.
Hata hivyo, Mukwala na Ateba ambaye aliongezwa kabla ya dirisha kufungwa mwanzoni mwa msimu, bado wanakabiliwa na changamoto ya kutengeneza nafasi na kufunga mabao, hali inayomfanya kocha na benchi la ufundi kujiuliza namna bora ya kuwaongezea ufanisi wa ushambuliaji.
Akiongelea viwango vya washambuliaji wake wa kati, kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema; “Nahitaji kuona wote wakiwa kwenye viwango bora, kuhusu kucheza kila mmoja atatumika kulingana na mpango wa mechi husika.”
Kwa upande wa Yanga, hali si nzuri sana. Washambuliaji wao wa kati, ambao ni Prince Dube, Clement Mzize, Jean Baleke na Kennedy Musonda, wana jumla ya mabao matatu pekee kwenye michezo ya ligi waliyocheza. Dube hajafunga bao lolote msimu huu, huku Mzize, Baleke, na Musonda kila mmoja akiwa na bao moja tu.
Hali hii imezua changamoto kubwa kwa Yanga, ambao msimu uliopita walikuwa na safu bora ya ushambuliaji. Hii ina maana kuwa washambuliaji hao wote watatu wamemzidi beki wa timu hiyo Ibrahim Hamad Bacca kwa bao moja tu.
Mabao machache kutoka kwa washambuliaji wa timu hiyo yameleta presha kwa wachezaji hao, huku kocha Miguel Gamondi akibaki na jukumu la kuwapa motisha na kuwaweka kwenye kiwango cha juu ili kufikia malengo ya msimu.
Katika moja ya mahojiano yake, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema; “Nafurahia kiwango cha timu yangu, nina washambuliaji wazuri ambao kila mmoja tunahitaji mchango wake kwa asilimia 100.”
Huko Azam mambo siyo mabaya
Azam FC nao wanakabiliwa na hali kama hiyo. Washambuliaji wao wa kati, Jhonier Alfonso Blanco, Nassor Saadun, na Franklin Navarro, wanaonekana kuwa na changamoto ya kufunga mabao. Hadi sasa, Blanco ana bao moja, Saadun ana mabao matatu, na Navarro hajafunga bao lolote.
Azam walitarajia kuona Blanco na Navarro wakiimarisha safu ya ushambuliaji, lakini hadi sasa, matumaini hayo bado hayajazaa matunda. Hali hii inawafanya Azam kuhitaji mabadiliko ya haraka, hasa kwenye eneo la ushambuliaji, ili waweze kufanikisha malengo yao ya msimu huu.
Kutokana na changamoto iliyopo kwa Azam katika eneo la mwisho la ushambuliaji, imembidi kocha wa kikosi hicho, Rachid Taoussi imebidi kumtumia Saadun ndio angalau anaonekana kuziba pengo hilo.Saadun sio mshambuliaji wa mwisho kiasili ni mzuri akishambulia kutokea pembeni au kuwa mshambuliaji wa pili.
Sababu mbalimbali zinaweza kuwa zimechangia kupungua kwa ufanisi wa washambuliaji wa Simba, Yanga, na Azam msimu huu.
Kwanza, kunaweza kuwa na changamoto kwenye mifumo ya uchezaji. Pia, presha kubwa kutoka kwa mashabiki na matarajio ya timu yanaweza kuwa na athari kwa wachezaji hao.
Pia, inaweza kuwa suala la majeraha na uchovu, ambapo baadhi ya wachezaji wamekuwa wakikumbana na majeraha ya mara kwa mara au kutofanya mazoezi ya kutosha, hali inayowaathiri katika kuonyesha kiwango bora uwanjani.
Wakati washambuliaji wa kati wa Simba, Yanga na Azam wakikabiliana na wakati mgumu, hali ni tofauti kwa mzawa, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ akiwa na Fountain Gate kabla ya mchezo wa jana, ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora kwenye ligi akiweka kambani mabao sita.
Idadi ya mabao sita ambayo yamefungwa na washambuliaji wote wa kati wa Simba ndio aliyofunga Gomez. Kwa Yanga mabao yao matatu ni nusu yake tu kama ilivyo pia kwa Azam FC, lakini mchezaji wa pili kwa kufunga Edgar Williams ambaye naye anatokea Fountain na wote wakiwa wazawa.
Kocha wa zamani wa Yanga na Azam FC, Hans van der Pluijm alisema; “Mpira siku hizi umebadilika na hata washambuliaji wa mwisho kabisa kiasili wameanza kupotea, wapo makocha ambao wanaweza kumtumia mfumo fulani ambaye hafungi mabao lakini anatoa zaidi ya kile ambacho kinahitajika, kwanini? labda uwepo wake unatoa nafasi ya wengine kufunga hilo, nalo linatakiwa kutazamwa.”
Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina, Mohamed Badru alisema: “Simba na Yanga inawashambuliaji wazuri sana lakini nadhani wamekuwa na majukumu mengi uwanjani ambayo yanaathiri jukumu lao mama la kufunga, nadhani wanatakiwa kuwa tayari kubeba majukumu mengine ya kiufundi huku wakitekeleza kwa kufanyika kazi pia namna ya kutumia nafasi.”