Bei ya petroli, dizeli zashuka Dar, Tanga

Dar es Salaam. Wanunuzi wa rejareja wa mafuta ya petroli na dizeli yanayopitia Bandari za Dar es Salaam na Tanga wataendelea kupata ahueni zaidi, baada ya bei kutangazwa kupungua Novemba mwaka huu ikilinganishwa na zilizokuwapo Oktoba.

Bei zimeendelea kushuka, licha ya gharama za uagizaji mafuta kutoka soko la Uarabuni kupungua kwa upande wa petroli pekee kwa wastani wa asilimia 3.91, huku gharama za dizeli zikiongezeka kwa asilimia 14.4 katika Bandari ya Dar es Salaam.

Katika Bandari ya Mtwara, gharama za uagizaji mafuta zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 0.67 kwa petroli na dizeli.

Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) iliyotolewa leo Jumatano Novemba 6, 2024 inaonyesha petroli kwa rejareja inayopitia Bandari ya Dar es Salaam itauzwa Sh2,943 kwa lita, dizeli Sh2,844 na mafuta ya taa Sh2,943.

Bei ya petroli ni pungufu kutoka Sh3,011 iliyouzwa Oktoba mwaka huu na Sh2,846 kwa dizeli mwezi uliopita, huku mafuta ya taa yakiendelea kubaki yalipokuwa.

Kwa Bandari ya Tanga, bei ya rejareja ya petroli itakuwa Sh2,948 kutoka Sh3,016 mwezi uliopita, dizeli itauzwa Sh2,855 kutoka Sh2,859 na mafuta ya taa yakisalia kuwa Sh2,989.

Kwa wanunuzi wa rejareja watakaotumia mafuta yanayopita Bandari ya Mtwara watanunua lita moja ya petroli kwa Sh3,015 ikiwa ni ongezeko la Sh1 kutoka bei iliyokuwapo Oktoba, dizeli itanunuliwa kwa Sh2,916 kutoka Sh2,862 na mafuta ya taa yakibaki kuwa Sh3,016.

Kwa wanunuzi wa jumla, mafuta ya petroli yatakayopitia Bandari ya Mtwara yatauzwa Sh2,811 kutoka Sh2,880, dizeli ikitoka Sh2,714 za Oktoba mwaka huu hadi Sh2,712, huku mafuta ya taa yakiwa Sh2,812 kama ilivyokuwa awali.

Ewura imezitaka kampuni za mafuta kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani, isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022.

Pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionyesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imesema taarifa ya Ewura iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Dk James Mwainyekule.

Ewura imesema kutofanya hivyo adhabu itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wametakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP), huku wanunuzi wakitakiwa kuhakikisha wanapata stakabadhi hizo.

Stakabadhi hizo zinatakiwa kuonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

“Stakabadhi zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa. Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli,” imeeleza taarifa hiyo.

Related Posts