Lindi/Mtwara. Baada ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kutoa vibali vya dharura kwa mabasi kupita njia ya Songea wakitokea Lindi na Mtwara, hali ni tete kwa Mkoa wa Lindi huku mkoa wa Mtwara ukitoa zaidi ya mabasi matatu kupitia njia hiyo.
Mamlaka hiyo ilitoa ruhusa kwa dharura kwa wasafirishaji ambao ratiba zao zimeathiriwa na uharibifu wa barabara ya Dar es Salaam – Lindi uliosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na hivyo kupendekeza kutumika kwa barabara ya Songea – Makambako – Iringa.
Mabasi yanayotokea Mtwara yanapita njia ya Masasi – Songea ambapo nauli ni kati ya Sh105,000 hadi Sh109,000 huku usafirishaji mkoa wa Lindi, ukiwa umesimama kutokana na mabasi mengi kuanzia safari zao mkoani Mtwara.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, mmoja ya wamiliki wa mabasi walioruhusu magari yao kusafiri kupitia Songea, Abdulkarim Masoud anayemiliki mabasi ya King Yasin, amesema kutokana na dharura, amelazimika kutoa gari lake ili kusaidia jamii.
Amesema baada ya kuona magari mengine yakipita Songea, aliiona ni fursa, hivyo amelazimika kutoa gari ambalo limeondoka saa 12 asubuhi ya leo.
“Basi limeondoka leo saa 12 asubuhi na abiria tumewapata, hii njia ni mbali lakini hakuna namna hii ni dharura. Kuna wagonjwa, kuna watoto sio wote wenye uwezo wa kumudu nauli za ndege ili kusaidia watu,” amesema.
Amesema alipata wazo baada ya kuona mabasi mengine mawili yakipita huko, hivyo amesema fursa ni kubwa lakini ni sehemu ya kutoa huduma ingawa mvua hizi zimewaathiri.
“Yaani hata hawa abiria tuliopata leo hatutegemei kwa kesho kuwapata, ina maana tunaenda kupunguza mapato, hivyo hali ya usafirishaji itazorota. Tunaomba saa 72 barabara zikamilike ili tuendelee na maisha yetu ya kawaida,” amesema Masoud.
Kwa upande wake, Said Juma, mkazi wa Lindi mjini, amesema magari yamesimama kwa kuwa magari mengi yanayoenda Dar es Salaam huanzia mkoa wa Mtwara, hivyo kwa Lindi kwa sasa hakuna basi la dharura.
“Wapo wenye uhitaji lakini hawawezi kumudu gharama za kwenda kuanzia safari Mtwara, utakuwa ni mzunguko mkubwa. Jana, kuna basi moja tu la kampuni ya Baraka Classic, ndiyo lililoanza safari kutokea hapa Lindi kupitia barabara ya Masasi – Songea,” amesema Juma.