KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema sababu za kuanza taratibu kucheka na nyavu katika Ligi Kuu Bara msimu huu zinatokana na namna alivyobadilishiwa majukumu ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Mmoroco, Rachid Taoussi.
Fei Toto ambaye msimu uliopita alikuwa akifanya majukumu ya washambuliaji, alifunga mabao 19 nyuma ya kinara Stephane Aziz Ki aliyemaliza na 21.
Msimu huu kiungo huyo katika mechi kumi, ametupia bao moja na kutoa asisti nne wakati msimu uliopita mechi ya kwanza pekee alifunga mabao matatu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto alisema suala la kufunga linakuja kwa kutumia nafasi na hakuna kinachoshindikana endapo atapata nafasi hizo licha ya kwamba sasa amepewa jukumu lingine la kuwatengenezea washambuliaji wa mwisho.
“Ukiangalia nafasi niliyokuwa nacheza msimu uliopita nikifunga idadi kubwa ya mabao ni tofauti na msimu huu ambao nacheza nyuma ya washambuliaji.
“Mimi ni mchezaji, naweza kucheza nafasi yoyote, kikubwa kocha aniamini tu, nafurahi kupata nafasi kikosi cha kwanza bila kujali wapi nimepangwa, majukumu mapya nayafanya kwa usahihi na ndio maana nimefanikiwa kutoa asisti nne,” alisema Fei Toto
Akizungumzia ligi kwa ujumla, Fei Toto alisema ni ngumu lakini jitihada, mbinu na ubora wa kikosi ndio umekuwa ukiamua matokeo, huku akiamini kwamba timu yake itamaliza nafasi nzuri itakayofanya msimu ujao kushiriki tena michuano ya kimataifa.
“Msimu huu ni mgumu, timu nyingi zimeanza vyema na kuonyesha ushindani, nafikiri maandalizi mazuri, ubora wa kikosi na mbinu nzuri za makocha ndio zinachangia matokeo mazuri,” alisema.
“Licha ya ugumu uliopo, tuna imani kubwa ya kurudi kimataifa msimu ujao na hilo linawezekana kutokana na aina ya kikosi na benchi la ufundi tulilonalo.”
Msimu uliopita wakati Fei Toto anamaliza ligi na mabao 19, alikuwa akichezeshwa kama mshambuliaji wa mwisho kutokana na eneo hilo kukumbwa na majeruhi wengi akiwemo Franklin Navarro na Alassane Diao, lakini msimu huu uwepo wa Nassor Saadun, Jhonier Blanco na Adam Adam inamlazimu Fei Toto kurudi kwenye majukumu yake halisi ya kiungo mshambuliaji.