Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Usajili wa Leseni za Biashara (BRELA), Shirika la Miliki Ubunifu ‘Duniani World Interllectual Property Organization’ (WIPO), Shirika la Miliki Buinfu Kanda ya Afrika (ARIPO)na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) wanatoa mafunzo kwa wakufunzi watakaokuwa na jukumu la kufundisha wadau mbalimbali kuhusu umuhimu na faida ya miliki bunifu ili kuleta chachu ya maendeleo.
Mafunzo hayo yamejumuisha washiriki kutoka nchini mbalimbali za Afrika ikiwemo mwenyeji, Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi, Namibia, Zambia, Botswana, Rwanda na nyinginezo lengo likiwa kuwapa elimu kuhusu Miliki Bunifu ambayo watakwenda kuwafundisha wadau mbalimbali katika nchi zao.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa akizungumza leo katika ufunguzi wa mafunzo hayo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema eneo la Miliki Bunifu limekuwa na changamoto kwa Bara la Afrika jambo ambalo limeshawi kushirikiana kutoa elimu hiyo ili kuchochea ufanisi katika sekta hiyo yenye utajiri mkubwa.
“Eneo hili la ubunifu bado lina changamoto kidogo kutokana na wadau husika kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu miliki bunifu kwa maana wapo wanakuja na bunifu zao zikiwa hazina sifa, zingine zinatakiwa kurekebishwa ili ziwe na sifa stahiki.
“Na nyingine zina sifa lakini wahusika hawajui wapi kuzirasimisha ili kupata mafanikio kupitia kazi zao, kwani bunifu ni ajira na ni utajiri ikiwa zitarasimishwa ndiyo sababu Brela kwa kushirikiana na ARIPO na wadau wengine tukaamua kwa pamoja kutoa elimu hii ili nao wakafundishe wengine,” amesema.
Ameongeza kwamba anaamini baada ya mafunzo hayo washiriki watakwenda kutawanya elimu kuhusu Miliki Bunifu na itasaidia kufahamika zaidi kwa wadau katika mataifa ya Afrika na dunia kwa ujumla na kuleta tija stahiki na kuwa chachu ya maendeleo ya kukuza uchumi kama ambayo nchi zilizoendelea zinafanya.
Pia amefafanua kwamba WIPO ndio msimamizi mkuu wa Miliki Bunifu Duniani na wameona changamoto ya kuwepo upungufu wa ufahamu wa wadau kuhusu miliki bunifu katika nchi za dunia ya tatu na ni dhahiri mafunzo hayo yatakuwa sehemu ya kufanya vizuri kupitia miliki bunifu, Afrika na dunia kwa ujumla.
Ameongeza kwamba majaji na mawakili nao wameshiriki katika mafunzo hayo lengo ni kusaidia kutoa haki pindi kesi zinazohusu Miliki Bunifu zitakapokatiwa rufaa na kupelekwa Mahakama Kuu.
“Brela ikishatoa maamuzi katika mgogoro unaohusu Miliki Bunifu na ikikatiwa rufaa na kwenda Mahakama Kuu, ikiwa majaji hawana uelewa kuhusu Haki Bunifu inaweza kuleta shida kwenye maamuzi ndio maana nao tumewashirikisha katika elimu hii ili wapate kujifunza namna ya kutoa haki,”amesema.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Prof Willam Anangisye ambao ndio wenyeji wa mafunzo hayo ambayo yameanza leo, chuoni hapo na yanatarajiwa kufikia tamati Novemba 8 mwaka huu, amebainisha kwamba dunia ni kama kijiji hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa wadau ili wakaitoe kwa wengine na kuleta tija stahiki.
“Tunatoa elimu hii ya Miliki Bunifu kwa wenzetu ili waende wakaifundishe kwao ili itumike kulinda bunifu zao na tutafundisha kupitia tafiti zetu ambazo zimefanywa hapa Chuo Kikuu, watu wengi wamekuwa wakifanya tafiti na kuzifungia kabatini, kwa sasa tunataka tafiti zetu ziwe bidhaa kwa ajili ya biashara,” amesema.
Pia Kiongozi MKuu kutoka ARIPO,Outle Rapuleng, amesema katika ushirikiano wao kati yao na Brela na wadau wengine katika semina hiyo imekuja baada ya kuona kuna uelewa mdogo kwa wabunifu kutoka nchi zinazoendelea hususan Afrika.
“Naamini elimu tunayoitoa hapa kwa siku hizi chache zitasaidia kupata wakufunzi wengi ambao watakwenda katika maeneo yao na kusambaza elimu kuhusu miliki bunifu itakayosaidia kuwepo kwa uwelewa mkubwa kwa wajariamali na kuleta mafanikio yanayotakiwa kupitia tasnia ya miliki bunifu, “amesema.
Mohamed Ali Maalim, kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali Zanzibar (BPRA), kwa upande wake ameweka wazi kuwa elimu ambayo watapata watakwenda kuwafundisha wabunifu katika maeneo yao ili wazitumie kujiletea maendeleo kama maana miliki bunifu ni mali kama mali nyingine.
“Elimu tutakayoipata hapa tutakwenda kuitoa kwa wadau wengi zaidi itakayowasaidia kulinda mali zao na kujipatia fedha na kuwa kichocheo kwao kufanya bunifu nyingi zaidi kwa ajili ya kujitengenezea kipato kwani kwa sasa inaonekana wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu miliki bunifu na ndio maana leo tunapewa elimu hii ili tukaisambazae kwa wengine,” amesema.