Fadlu: Nashusha vyuma hivi Simba dirisha dogo

SIMBA inacheza leo dhidi ya KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara. Lakini hesabu za kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids ziko kwenye dirisha dogo. Ameweka wazi kwamba Desemba lazima asajili wachezaji wapya watatu ambapo mmoja tayari wameshamalizana nae na yupo Dar es Salaam. Simba inapiga hesabu nzito kuongeza nguvu eneo la beki wa kati na kiungo mshambuliaji mmoja dirisha lijalo ambao wanahitajika na kocha Fadlu aliyetua hivi karibuni kutoka Raja AC ya Morocco.

Simba inaendelea na msako wa mshambuliaji gani wamchukue ndani ya siku chache zilizosalia kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili huku wakiwa tayari wamemalizana na winga mwenye kasi Elie Mpanzu.

Disemba 16 mwaka huu ndio tarehe ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili na linafungwa Januari 15 mwakani kwa kila timu inahaha kukamilisha maeneo hayo muhimu kulingana na mapungufu waliyonayo.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa, licha ya kocha Fadlu kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji, lakini bado hajaridhishwa na nyota waliopo hasa eneo la kiungo mshambuliaji ameomba kutafutiwa nyota mmoja eneo hilo.

Chanzo hicho kimesisitiza kuwa kikosi chao kitafunga usajili kwa kuwaingiza wachezaji wawili kiungo mshambuliaji mmoja na beki wa kati ambaye atasaidiana kwa usahihi na Fondoh Che Malone na Abdulrazack Hamza wanaotumika sana licha ya kuwepo pia Hussein Kazi na Chamou Karaboue.

“Eneo la ushambuliaji limekosa kiungo anayeweza kusambaza pasi ambazo zinaweza kuwa na madhara kwa wapinzani na faida kwa mchezaji wa mwisho hilo amelisisitiza sana,” kilisema na kuongeza chanzo hicho;

“Ni mapema sana kuzungumza masuala ya usajili, lakini kocha licha ya kwamba anajenga kikosi hajaridhishwa na maeneo hayo matatu ambapo eneo moja tayari limefanyiwa kazi kwa kuongezwa Mpanzu.”

Mwanaspoti lilipomtafuta kocha Fadlu, alikiri ni kweli Simba inahitaji kuimarishwa zaidi ili kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

“Tumeona ni wapi tunahitaji kuongeza nguvu. Tunatambua kuna dirisha dogo linakuja na ni lazima tutilie mkazo kuleta wachezaji watakaotusaidia kufika kwenye kiwango cha juu zaidi,” alisema Davids kwa msisitizo.

Katika eneo la kiungo cha ushambuliaji namba 10, Simba ina Charles Ahoua na Awesu Awesu tu, huku wengine wakiingia na kutoka ambao wanatumika zaidi eneo namba nane na mawinga walio wengi zaidi.

Hii ni ishara ya wazi Simba inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kukabiliana na presha, uzoefu wa mechi kubwa, na wanaoweza kuleta matokeo pale inapohitajika zaidi.

Mpanzu ambaye tayari ameanza programu za kikosi hicho anatarajiwa kuwa miongoni mwa silaha muhimu za Fadlu zitakazoingia wakati wa dirisha hilo, usajili wa winga huyo kutoka AS Vita Club ya DR Congo ulichelewa hivyo itambidi kusubiri hadi dirisha la usajli litakapofunguliwa. Simba imepania kurejea kwenye ubora wao ambapo katika kipindi kifupi wamefumua sehemu kubwa ya kikosi chao ili kufanya vizuri kimataifa na hata katika ligi ya ndani ambako wamejikuta wakiachia mataji mengi.

Related Posts