KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars‘, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ameita kikosi cha wachezaji 26 watakaoingia kambini kesho kwa ajili ya michezo miwili ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), itakayofanyika mwakani Morocco, huku beki wa Simba, Shomari Kapombe akijumuishwa.
Stars iliyopo kundi ‘H’ ina kibarua cha kupambana na Ethiopia ugenini Novemba 16, huku ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa suluhu mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam Septemba 4, mwaka huu.
Baada ya hapo itamalizia mchezo wa mwisho dhidi ya Guinea, Novemba 19, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikikumbukwa kwamba ule wa awali iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, Septemba 10, mwaka huu.
Akizungumzia wachezaji hao, Morocco amesema sababu kubwa ya kumjumuisha Manula ni kutokana na uwezo aliouonyesha katika michezo miwili iliyopita ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani maarufu Chan.
“Ni kweli Manula amekuwa hana michezo mingi ya ushindani, lakini baada ya kumuona katika mechi hizi mbili na Sudan tumeona anaweza pia kutuongezea kitu cha ziada kwa wote waliopo,” amesema kocha huyo.
Morocco ameongeza kuwa kwa nyota wengine wapya ambao hawakucheza michezo iliyopita wamepata nafasi hiyo kutokana na uwezo waliouonyesha katika klabu wanazocheza.
“Kapombe na wengine wamestahili pia kuwepo kwa sababu hii ni timu ya taifa na yeyote anayeonyesha uwezo mkubwa anastahili kuwepo. Matumaini yetu ni kuona tunafuzu Afcon mwakani ndio maana tumeita kikosi bora cha kutimiza malengo hayo.”
Nyota wengine wapya waliojumuishwa ni mshambuliaji Saimon Msuva ambaye alikosekana katika michezo miwili iliyopita sambamba na beki wa Simba, Abdulrazack Hamza aliyekuwa majeruhi.
“Hamza ni majeruhi lakini ameanza mazoezi, tulizungumza naye na jopo la madaktari tukaona anaweza akacheza kwa sababu tuna siku sita zaidi huko mbeleni.”
Wachezaji walioitwa ni makipa, Aishi Manula (Simba), Ziberi Foba (Azam FC) na Metacha Mnata wa Singida Black Stars huku mabeki wakiwa ni Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Abdulrazack Hamza (Simba), Lusajo Mwaikenda na Pascal Msindo wa Azam FC.
Wengine ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, (Yanga), Ibrahim Ame (Mashujaa) na David Bryson kutoka JKT Tanzania.
Viungo ni Adolf Mtasingwa, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Nassor Saadun (Azam FC), Mudathir Yahya (Yanga), Kibu Denis (Simba), Novatus Dismas (Goztepe), Habib Khalid (Singida Black Stars) na Abdulkarim Kiswanya (Azam FC U-20).
Washambuliaji ni Mbwana Samatta (PAOK), Cyprian Kachwele (Vancouver Whitecaps), Clement Mzize (Yanga), Idd Seleman ‘Nado’ (Azam FC), Ismail Mgunda (Mashujaa) na Simon Msuva (Al-Talaba).
Katika kundi la ‘H’, linaongozwa na DR Congo yenye pointi 12, ikifuatiwa na Guinea yenye sita huku Stars ikiwa ya tatu baada ya kukusanya pointi zake nne.
Ethiopia inaburuza mkia wa kundi hilo ikiwa na pointi moja tu, baada ya kila timu kucheza jumla ya michezo minne hadi sasa.
Timu hiyo imeshiriki AFCON tatu tofauti ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa ya Nigeria mwaka 1980, kisha ikapata nafasi hiyo tena baada ya miaka 39, ya kushiriki ilipofanya hivyo mwaka 2019, Misri chini ya Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike.
Mara ya tatu ilikuwa mwaka huu wa 2024 kule Ivory Coast ikiwa na Kocha Mkuu, Adel Amrouche ambapo ilipangwa kundi ‘F’ lililokuwa na timu za taifa za Morocco, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuishia hatua ya makundi.