Arusha. Wito wa kuongeza watafiti wanawake umetolewa kwa nchi za Afrika ili kupunguza vikwazo ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, ukosefu wa upatinakaji wa fedha za ruzuku za utafiti.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Sayansi ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), mwaka 2021 ni asilimia 33 tu ya watafiti wanawake duniani.
Hayo yamebainishwa Jumanne Novemba 5, 2024 na Jaji wa Mahakama ya Juu nchini Uganda, Profesa Lilian Ekirikubinza wakati wa uzinduzi wa mkakati mpya kwa ajili ya wanawake watafiti barani Afrika.
Uzinduzi huo umefanyika katika kongamano la nane la vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika la YouLead.
Jaji huyo amesema ongezeko la wanawake wengi wanaofanya utafiti katika nyanja mbalimbali utawezesha kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii.
Ametaja malengo ya ilani hiyo ni kujenga ufahamu wa kukosekana usawa na changamoto wanazokabiliana nazo wanawake katika utafiti na kutoa mapendekezo kwa wadau mbalimbali ikiwemo Serikali.
Ametaja miongoni mwa mapendekezo hayo ni Serikali kuanzisha sera za kuhakikisha angalau asilimia 30 ya wanawake katika nafasi za utafiti ili kusaidiai kuziba pengo la jinsia katika utafiti.
“Ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika utafiti lazima tupinge mifumo dume ambayo inatawala jamii zetu na licha ya idadi kubwa ya wanawake kupata elimu za juu, bado idadi ya watafiti wanawake ni ndogo hasa katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.”
“Wanawake wanakabiliwa na vikwazo vingi vya kimaendeleo katika utafiti, ikiwemo sera za taasisi zingine zisizozingatia jinsia, ukosefu wa upatikanaji za ruzuku za utafiti, mitazamo ya kijinsia na mazingira ya mifumo dume,” amesema Jaji huyo.
Amesema mwezi Machi mwaka huu, wanawake watafiti 50 kutoka nchi 12 barani Afrika, walikutana na kujadili namna ya kuhusu mkakati huo wa kuongeza idadi ya wanawake katika utafiti kwenye nchi za Afrika.
Mkuu wa Kitengo cha Taaluma kutoka Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Dk Irene Lugala amesema wameona katika Vyuo Vikuu mbalimbali kuna asilimia ndogo ya wanawake wanaofanya tafiti.
“Tunataka tutengeneze role models wengi na tukiwa na wanawake wanaofanya tafiti, tutawafanya wasichana wadogo wajifunze na wao waige mfano huo, tunaomba kuwe na mazingira rafiki na shirikishi ya kumuwezesha mwanamke anayefanya utafiti,” amesema.
Kuhusu kongamano hilo la vijana, Dk Irene amesema limekuwa na mchango mkubwa hasa katika maendeleo ya vijana kushiriki katika kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo siasa.
“Kongamano hili linaleta vijana kutoka nchi za Afrika Mashariki na nchi zingine za afrika, kujadili masuala mbalimbali ikiwemo ya uongozi, kiuchumi na tumewasikia hapa asubuhi wakisisitiza kupewa nafasi kwenye ngazi za maamuzi katika masuala yanayohusu vijana,” amesema.
Amesema viongozi wengi wakiwa vijana katika nchi za Afrika itasaidia kukusanya sauti zao na kutatua changamoto zinazokabili kundi hilo.
Awali Mkuu wa Idara za Mafunzo MS TCDC, Said Omar, amesema kongamano hilo la mwaka ni la nane kufanyika ambapo kongamano la kwanza lilifanyika mwaka 2017 na kushirikisha vijana kutoka nchini Tanzania pekee.
Amesema kuanzia mwaka 2018 kongamano hilo linafanyika na kushirikisha vijana kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi nyingine za Afrika.
Amesema kwa mwaka huu kongamano hilo limeshirikisha vijana 300 na mwaka huu linaongozwa na kauli mbiu ya kuhamasisha vijana kuona umuhimu wa elimu katika muktadha wa maendeleo barani Afrika.
“Vijana hawa watakuwa hapa kwa siku tano wakizungumzia masuala ambayo yanawahusu, kuibua fursa zilizopo hasa katika nyanja za kimaendeleo na masuala mengine,” amesema.
Balozi wa Vijana wa EAC, kutoka nchini Tanzania, Hope Kacheri amesema kwa mwaka huu wanatarajia kujadili namna elimu inavyoweza kumkomboa kijana ikiwemo katika suala la ajira na kuwa kupitia baraza hilo wamekuwa wakisisitiza vijana juu ya suala hilo muhimu.
Amesema wanaamini teknolojia ina mchango mkubwa hasa kwa kundi la vijana na kutaja moja ya changamoto zinazokwamisha vijana kushindwa kufikia malengo yao ni pamoja na kukosa msukumo kwa sababu ya kutegemea ajira.