Amesisitiza kuwa viongozi na wanachama wa CCM watakaopata fursa ya kuzungumza katika majukwaa ya kisiasa katika kampeni za uchaguzi huo, watajikita kueleza maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Rais Dk. Samia katika ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa.
Makalla aliyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, wakati akizungumza na maelfu ya wanachama na viongozi wa CCM Wilaya ya Ilala kwenye ukumbi wa Mwigo Tabata,ambapo alitumia fursa hiyo kuelelezea msimamo wa CCM kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
“Tujenge hoja na tutofautiane kwa itikadi kwani tuna Tanzania moja. Uchaguzi uiache Tanzania ikiwa moja yenye amani na utulivu. CCM tunavyosema ndiyo tunamaanisha.
Makalla alisisitiza: “Kwa mambo yaliyofanywa na Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kila mwanaCCM akipewa nafasi ya kuongea jukwaani ataongea mambo mengi yaliyofanywa. Kwa hiyo kwetu sisi matusi, kejeli haitokuwa sehemu yetu.”
Alitoa maagizo kwa viongozi wa Chama kuanzia mabalozi kufanya kampeni ya kuhamasisha wananchi waliojikindikisha katika daftari la mkazi, kujitokeza kupiga kura ifikapo Novemba 27 mwaka huu.
Alibainisha kuwa uandikishaji wapiga kura ulikuwa mzuri kwa sababu kuanzia mabalozi, matawi, kata, wilaya, mikoa na uratibu wa taifa, kazi kubwa ya uhamasishaji ilifanyika.
“Kuanzia tarehe 21 Novemba, muaze kuwakumbusha wananchi wajitokeze kupiga kura. CCM kimetoa tamko kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa kwamba inaamini kwamba ili ushike dola kwa mfumo wa uchaguzi wa Tanzania, lazima ushinde serikali za mitaa na baadaye ushinde uchaguzi mkuu,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Makalla amempongeza Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu kwa kueleza ukweli kuhusu chama hicho kushindwa kusimamisha wagombea katika kila eneo la uchaguzi.
Alisema Lissu amekuwa mkweli kuliko mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye aliwatishia viongozi wa CHADEMA kwamba endapo wakishindwa kusimamisha wagombea katika kila eneo, watafukuzwa.
“Jana, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu alisema hawawezi kwa hali iliyopo kusimamisha mgombea kila sehemu, Tundu Lissu nampongeza kwa sababu amekuwa mkweli kuliko mwenyekiti wake.
“Mwenyekiti wake aliwaita viongozi wake Dar es Salaam akawaambia kiongozi yeyote ambaye hatosimamisha mgombea katika kitongoji, kijiji na mitaa, atawafukuza. Sasa nataka uwafukuze kwa sababu Tundu Lissu amekiri haiwezekani na hawajasimamisha wagombea kila sehemu,” alieleza.
Makalla alisema tafsiri ya chama hicho kutosimamisha wagombe ni kwamba hakipo tayari kushika dola.
“Dola haishikwi kwa kuweka wagombea wachache, CCM ipo tayari na imethibitisha kwa vitendo kwa kuweka wagombea kila sehemu, tupo yatari kushika dola,” alifafanua Makalla.