BEKI wa kushoto wa Tabora United, Salum Chuku atakuwa nje ya uwanja kwa kwa zaidi ya miezi minne akiuguza jeraha la goti alilolipata Septemba 14, mwaka huu, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Chuku amerejea Ligi Kuu msimu huu alipojiunga na Tabora United kwa mwaka mmoja akitokea Mwadui (sasa Bigman FC) iliyokuwa First League baada ya kuipandisha daraja (Championship) msimu uliopita.
Majeraha hayo ni pigo kwa mchezaji huyo wa zamani wa Toto Africans, Singida, KMC, Mbeya Kwanza na Nkana ya Zambia, kwani ni muda mfupi ametoka kwenye majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa miaka miwili kabla ya kurejea msimu uliopita akiwa nahodha wa Mwadui FC.
Tayari nyota huyo ameshazikosa mechi sita dhidi ya Fountain Gate, KenGold, Dodoma, JKT Tanzania, Pamba Jiji na Mashujaa FC na kabla ya majeraha hayo alianza kwenye michezo minne dhidi ya Simba, Kagera Sugar, Tanzania Prisons na Namungo akifunga bao muhimu katika ushindi wa 2-0 mkoani Lindi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chuku alisema anatarajia kufanyiwa upasuaji mdogo wa jeraha hilo kwenye goti chini ya uangalizi wa madaktari wa timu huku akiamini hajakata tamaa, kwani kiu yake yake ni kucheza Ligi Kuu na kuisaidia timu.
“Hali bado. Ndiyo nataka nifanye matibabu Novemba 10, kisha nitasikilizia. Naambiwa inaweza kuchukua miezi minne mpaka mitano kupona na kurejea uwanjani,” alisema Chuku.
Aliongeza; “Naona ni changamoto tu, naamini nitakaa sawa tena na nitarudi, siyo kinyonge yaani mimi narudi tu freshi, na naendelea kuwa karibu na timu na kutoa mchango wangu wa kushauri na hamasa kwa wenzangu.”