Wadakwa wakidaiwa kuhujumu miundombinu ya Tanesco

Tabora. Jeshi la Polisi mkoa wa Tabora linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa miundombinu ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) Mkoa wa Tabora.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 6, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema wanawashikilia watu saba wanaodaiwa kufanya matukio hayo katika maeneo tofauti.

Polisi katika Kijiji cha Nindo, Wilaya ya Nzega, Mkoa wa Tabora, wakishirikiana na maofisa wa Tanesco na wananchi, limefanikiwa kumkamata mtu mmoja kwa tuhuma za wizi wa waya za copper earthwire kutoka kwenye transfoma mbili.

“Askari walipokuwa wakiendelea na msako waligundua kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa tayari amefanya uharibifu na wizi kwenye transfoma nyingine tatu. Msako ulipoendelea katika maeneo tofauti, tulifanikiwa pia kuwakamata watuhumiwa wengine sita katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu ambao walikuwa wakishirikiana kutekeleza uhalifu huu,” amedai Kamanda Abwao.

Aidha, amesema katika msako huo jumla ya waya wa copa uliokamatwa ni armoured cable 6mmsq wenye kilo 28.7, bare copper conductor 35mmsq kilo tisa na mfuko wa misumali inchi mbili kilo 24.3 vyote vikiwa ni mali ya Tanesco na baadhi ya watuhumiwa wamekutwa na vifaa vinavyowawezesha kutenda uhalifu huo ambao ni viatu vya kupandia nguzo, msumeno wa kukatia chuma na nyundo.

Alipotafutwa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Tabora, Mhandishi Amina Mohamed kuzungumzia sakata hilo amesema umeme unapozima wanapata hasara kubwa.

“Ni kweli kwa wizi ambao umetokea kwenye Wilaya za Sikonge na Nzega tumepata hasara ya zaidi ya Sh4 milioni kwa kuwa zile waya ni za ulinzi ardhini ambazo ziliibiwa na ndio zilikuwa zinalinda transfoma,” amesema meneja huyo.

Amesema baada ya kufuatilia, wamebaini vishoka wanaofanya uhalifu huo ni miongoni mwa mafundi wanaopatiwa ajira za muda na mawakala wa umeme vijijini (REA).

“Wakimaliza muda wa kazi, huwa wanaondoka na vifaa hivyo, lakini Tanesco  kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tutaendelea kufanya oparesheni kali  ili kuondoa hali hii ambayo imeemdelea kutia hasara kwa shirika mara kwa mara,” amesema Mohamed.

Related Posts