Utafiti wa MUHAS Wabaini kuwa matumizi ya viuatilifu kwa wazalishaji wa mbogamboga na mazao ya chakula ni Makubwa

Mkuu wa Afya kazini kutoka Wizara ya Afya, Joseph Birago na Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Apolinary Kamuhabwa wakitoa zawadi kwa washiriki wa tafitiĀ  mbambali zilizofanyika nchini kote juu ya madhara ya viuatilifu kwa binadamu.

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

UTAFITI uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) umebaini matumizi makubwa ya viuatilifu kwa wazalishaji wa mbogamboga na mazao ya chakula ikiwemo korosho na nafaka.

Wanasema kuwa matumizi holela ya viuatilifu kwenye mazao ya chakula na mbogamboga, yanatajwa kusababisha magonjwa mbalimbali yakiwemo kupoteza uwezo wa kuzaa, saratani, shinikizo la damu na kisukari hivyo, wameshauri kufanyika kwa utafiti kubaini ukubwa wa tatizo hilo.

Hayo yamesemwa jijini Dae es Salaam leo na Mhadhiri Mwandamizi Kitengo cha Afya Kazini na Mazingira Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Vera Ngowi wakati wa kongamano la kujadili madhara ya viuatilifu kwa binadamu.

Ngowi amesisitiza kuwa wamefanya utafiti nchini kote na wamebaini watumiaji wakubwa wa viuatilifu ni wazalishaji wa mbogamboga, mazao ya nafaka na korosho.

Ameongeza kuwa mazao hayo ni ya chakula na kwamba hakuna anayepima kiasi cha viuatilifu vinavyotumika ili kudhibiti.

Ameeleza kuwa awali, wakulima wa mazao ya pamba na kahawa ndio walikuwa watumiaji wakubwa wa viuatilifu nchini lakini hali imebadilika.

“Kama tunakula mbogamboga zilizotumia viuatilifu vingi, si mpaka umwagiliie ndio udhurike, hata unapotumia kuna athari zake,” amesema.

Ngowi amesema ni vema kuchagua kiuatilifu cha kutumia ikiwemo kuachana na viuatilifu vya viwandani ambavyo vina madhara mengi na kulima kilimo hai.

Pia amesema haina maana kuwa kilimo hai hakitumii viuatilifu kabisa isipokuwa wanatumia viuatilifu vya asili ambavyo vinalinda afya.

“Wakati uchumi unakua, madhara ya afya yanaongezeka ikiwemo saratani, kisukari, shinikizo la damu na kupoteza uwezo wa kuzaa ambako kunahusishwa na viuatilifu,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa “Wizara ya afya na wanasayansi tuliangalie hili tatizo tuweze kufanya tafiti kujua mchango wa viuatilifu kwa uhakika kwenye magonjwa hayo, kwa kiasi gani ili

Amesema baada ya TPRA kufutwa hawafahamu ni taasisi gani ambayo inafanya utafiti kuhusu viuatilifu na kulinda afya za watu.

“Tunajadiliana kama chuo tuna mchango gani katika kusaidia anayedhibiti afya za watu kuhusu madhara ya viuatilifu kwenye ufundishaji na utafiti,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema kuwa wanaangalia maeneo mbalimbali ambayo yanaweza kuathiri afya za binadamu ikiwemo viuatilifu.

Ameeleza kumekuwa na changamoto za matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu kwenye mazao au wanyama licha ya wataalamu kuelekeza baada ya kutumia viuatilifu, kuwe na muda wa kusubiri dawa hizo zitoke kabla ya kutumiwa na binadamu.

“Kuna tatizo la uelewa au presha ya kutaka kuuza mazao haraka, kipindi cha kusubiri masalia ya viuatilifu yatoke hayazingatiwi, ni lazima kutoa elimu kwa wananchi,” amesisitiza

Profesa Kamuhabwa amesema matumizi mabaya ya viuatilifu ikiwemo viwango na aina ya viuatilifu hivyo, huweza kusababisha madhara ikiwemo magonjwa ya ngozi.

Vilevile amsema baada ya utafiti huo, lengo la ni kutoa mwongozo ili kudhibiti matumizi yasiyosahihi ya viuatilifu.

Naye, Mkuu wa Afya kazini kutoka Wizara ya Afya, Joseph Birago, ameeleza kuwa viuatilifu vimekuwa vikitumika kwenye kilimo na mifugo na kwamba yanapaswa kuzingatia afya ya jamii, mazingira, viumbe na mimea.

Amesema viuatilifu hutumika kuangamiza viluilui kwenye mazingira hivyo yakitumika vibaya, huathiri afya za binadamu na viumbe hai.

“Viuatilifu vimekuwa vikitumika kuzalisha mbogamboga ikiwemo nyanya na vitunguu lakini maelekezo yanapaswa yazingatiwe na jamii kwa matumizi bora ya viuatilifu,” amesema Birago.

Ameongeza kuwa ni lazima kuhakikisha wanakuwa na Tanzania salama wakati huu ambapo kuna mabadiliko ya tabia nchi.

Picha za Matukio mbalimbali.

Picha ya Pamoja.

Related Posts