Sh11.18 bilioni kusambaza umeme kaya 2,970 Shinyanga

Shinyanga. Kaya 2,970 katika Mkoa wa Shinyanga zinatarajia kufaidika na mradi wa umeme wenye thamani ya Sh11.18 bilioni unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Katika vitongoji 2,703 vya mkoa huo, ni vitongoji 930 pekee ambavyo tayari vina huduma ya umeme, huku vitongoji 1,773 vikiwa bado havijapata huduma hiyo.

Akizungumza leo Jumatano Novemba 6, 2024, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha wakati wa kumtambulisha mkandarasi wa mradi, Kampuni ya Derm Group (T) ya wazawa, Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Robert Dulle amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24, kuanzia Septemba 3, 2024, hadi Agosti 19, 2026, ukilenga kusambaza umeme katika vitongoji 90.

“Kwa niaba ya wananchi, tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha Shilingi 11,184,759,397.2 kitumike kupeleka umeme katika vitongoji 90 hapa mkoani. Leo tumekuja kumtambulisha mkandarasi, na tayari maandalizi ya utekelezaji wa mradi yameanza,” alisema Dulle.

Amsema mradi huo unalenga kugusa majimbo ya Shinyanga, Solwa, Kishapu, Msalala, Ushetu, na Kahama, huku kila jimbo litafaidika kwa vitongoji 15 kupatiwa umeme.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, alitoa pongezi kwa mradi huo akisema kuwa kukamilika kwake kutachochea shughuli za kiuchumi na maendeleo, zikiwemo viwanda, kilimo, na biashara.

“Pamoja na madini, Shinyanga tunajihusisha na kilimo cha mpunga. Tuna hamu ya kuona wakulima wakiongeza thamani ya mazao yao hapa vijijini kwa kusindika mpunga na kupata mchele, jambo litakaloongeza ajira na fursa nyingine za kiuchumi,” amesema Macha.

Amemhimiza mkandarasi kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa ubora na kukamilisha kwa wakati kama ilivyopangwa.

“Tunajivunia kuona kampuni za Kitanzania kama Derm zikiwa na uwezo wa kutekeleza miradi ya kitaifa. Pia tunatoa wito kwa mkandarasi kutumia huduma za watu wa maeneo ya mradi na kutoa nafasi za kazi kwa wananchi wa eneo husika,” amesema Macha.

Sophia John, mkazi wa Kata ya Didia wilayani Shinyanga, amesifu juhudi za Serikali za kusogeza huduma ya umeme vijijini, huku akisisitiza umuhimu wa kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati.

Iddi Shabani, mkazi wa Kata ya Ilola, alikubaliana na mawazo hayo, akisema kuwa mradi huu wa umeme utaimarisha maendeleo ya kiuchumi na kuinua maisha ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

“Niipongeze Serikali kwa kuleta mradi huo naamini utakuwa na manufaa makubwa kwa wanachi pindi ikikamilika kwa sababu itachochea hata baadhi ya watu kuanzisha viwanda na vitu vingine ambavyo vitakuwa na msaada katika jamii,” amesema Shabani.

Related Posts