Serikali kuwakopesha wajasiriamali 18.5bn/- kupitia NMB – MWANAHARAKATI MZALENDO

 

Na Mwandishi Wetu

Serikali imetenga kiasi cha TZS bilioni 18.5 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali nchini zitakazotolewa kama mikopo yenye masharti nafuu kupitia Benki ya NMB.

Makubaliano ya utaratibu wa ufadhili huo yalitiwa saini leo jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Bi Ruth Zaipuna, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe kwa niaba ya Serikali na kushuhudiwa na mkuu wa wizara hiyo, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima.

Akizungumza kabla ya utiaji saini ya mkataba huo wa miaka miwili, waziri huyo alisema wafanyabiashara wadogo na wa kati watakopeshwa fedha hizo kwa riba ya asilimia saba.

“TZS bilioni 18.5 ni hela nyingi za kuanzia lakini kiasi hiki kitaongezeka kwani lengo la Serikali ni kuifanya mikopo hii kuwa endelevu ili iwafikide watu wengi,” Dkt Gwajima alibainisha huku akisisitiza umuhimu wa kuitumia vizuri na kuirejesha kwa wakati.

Aliongeza kuwa fedha hizo zikiwekezwa vizuri zinaweza kuwa na tija kubwa kimaendeleo kwa kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha mapato ya kaya.

Dr Gwajima alisema mikopo hiyo ni sehemu ya utaratibu mpya wa Serikali kuyawezesha makundi maalum na kuhakikisha wanufaika wake ni wale tu waliolengwa kupata usaidizi huo.

“Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwa hiyo Serkali kupitia wizara hii ina kila sababu ya kuwakwamua na kuwawezesha ikiwemo kupitia mikopo hii nafuu ambayo NMB imeanza kuitoa leo.”

 

 

Kwa mujibu wa Dkt Shekalaghe utiaji saini na NMB kukopesha fedha hizo kumeitimisha mchakato wa wizara yao kuitafuta benki mshirika katika masuala mbalimbali ya kiutendaji na kimaendeleo.

Akibainisha kuwa mafungu ya mikopo hiyo nafuu itatoka kila mwaka, katibu mkuu huyo alisema Serikali imeanzisha utaratibu mpya wa kuyafadhili makundi maalumu na tayari uandikishaji ya wale wenye sifa stahiki umeanza na kwa upande wa wajasiriamali pia wanapewa vitambulisho maalum.

Katika maelezo yake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna alisema mkataba wa kutoa mikopo hiyo ni kielelezo cha jitihada kubwa zinazofanywa na benki hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wote nchini wakiwemo wale wadogo.
Aidha, alisema benki hiyo ina uzoefu na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wajasiriamali ambao umeifanya kutambulika kimataifa kama kinara wa kuzifadhili biashara changa, ndogo na za kati nchini.

“Tuzo tulizozipata mwaka huu katika hilo ni pamoja na zile za Benki Bora ya Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati na Benki Bora ya Uwezeshaji wa Biashara Ndogo na za Kati,” Bi Zaipuna alisema.

“Ukweli huo unadhihirishwa na idadi ya mikopo 129,540 yenye thamani ya TZS trilioni 2.03 iliyotolewa na NMB kwa wajasiriamali kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2023,” aliongeza na kueleza kuwa ukopeshaji huo kwa wajasiriamali wakiwemo wamachinga na boda boda ulikuwa ni wastani wa mikopo 2,699 kila mwezi na TZS bilioni 42.3 kwa mwezi.

“Historia ya Benki ya NMB imejengwa kupitia uwezeshaji wa sekta ya biashara ndogo na za kati, kutoa mikopo na juhudi za kuwafikia wafanyabiashara ni moja ya vipaumbele katika mpango mkakati wetu,” alifafanua.

Bi Zaipuna alimwambia Dkt Gwajima kuwa utiaji saini mkataba kati ya NMB na wizara yake kutapanua wigo wa kuwafikia wafanyabiashara wengi zaidi wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo nchini.

Pia alisema taasisi hiyo inajivunia kushirikishwa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika utekelezaji wa mipango ya kuwahudumia wajasiriamali kwa lengo la kukuza biashara zao na kuwapa fursa ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na pato la taifa kwa ujumla.

Akisisitiza umuhimu wa wajasiriamali katika maendeleo, Bi Zaipuna alisema shughuli zao ni zaidi ya asilimia 95 ya biashara zote rasmi duniani zikichangia asilimia 50 ya pato la taifa kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na zaidi ya asilimia 80 ya ajira zote barani Afrika.

“Pamoja na utoaji mikopo tunaamini kuwa wafanyabiashara hawa watafaidika pia na huduma nyingine mbalimbali za kifedha zinazotolewa na benki yetu na hivyo kuwafanya wakue kibiashara,” alibainisha huku akitilia mkazo umuhimu wa kuwapa elimu ya fedha ili kuhakikisha wanakuwa na nidhamu nzuri ya matumizi ya mikopo hiyo.

MWISHO…

Related Posts