Katika mfumo wa uchumi wa sarafu kidunia (fiat money system), fedha zilizo katika mzunguko zinaweza kupitia mabadiliko kadhaa kutokana na mwenendo wa kiuchumi, matumizi ya kila siku, na jinsi zinavyohifadhiwa na watumiaji. Hivyo, kutokana na mambo haya, uimara, uthabiti, na thamani yake yanategemea pia hali hizo.
Hivyo benki kuu kidunia, kama msimamizi wa mfumo wa sarafu, inahitaji hufanya maamuzi ya kubadili, kuongeza, au kupunguza kiasi cha fedha kilicho katika mzunguko kila baada ya muda fulani.
Mabadiliko katika mfumo wa sarafu yanaweza kuja kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, kuondoa fedha chakavu katika mzunguko ili kuleta mpya. Fedha ikiwa chakavu sana inaweza kutia shaka kwa watumiaji, na wengine wanaweza kwa hiari yao, kutoikubali katika kupokea malipo.
Fikiria unalipwa kwa noti ya Sh1,000 ambayo hata sifuri zake hazionekani vizuri. Katika msingi huu, kubadili sarafu kwa kuondoa chakavu na kuleta mpya kunaweza kusaidia kuongeza uwezo wa sarafu kwa kuifanya kuwa imara zaidi na yenye kuweza kudumu kwa muda mrefu, na kuifanya kuendelea kukubalika katika kufanya miamala. Mambo hayo, ni miongoni mwa sifa kuu za msingi za sarafu kwenye uchumi wa kisasa.
Sambamba na hilo, uondoaji wa sarafu kwenye mzunguko kwa maana ya kuondoa machapisho ya zamani na kuleta mpya, hata kama si chakavu, inaweza kuwa kinga katika mfumo wa sarafu ulivyo katika uchumi. Kadiri teknolojia inavyoendelea, mbinu za ulaghai katika utoaji wa fedha feki zinaweza kuibuka.
Kwa kuingiza fedha mpya katika mzunguko, kunatoa fursa za kuongeza alama mpya za kiusalama zilivyoboreshwa kama vile alama za maji, hologramu, rangi maalumu na nyinginezo. Hii inasaidia kudhibiti kiwango cha fedha kilichokatika mzunguko kuzuia fedha feki, na kufanya sarafu kuwa ya kuaminika katika matumizi.
Vilevile, kadiri uchumi unavyokuwa, thamani ya sarafu inabadilika na kupungua uwezo wake wa kununua. Katika hali hii, mabadiliko ya sarafu yanaweza kuja kwa mfano, kwa njia ya kuanzisha noti mpya ambazo hazikuwepo au kuondoa sarafu za zamani ambazo hazitumiki tena kwa sababu zimeshapoteza nguvu ya kimanunuzi.
Hivyo, mabadiliko ya sarafu katika namna hii yanaendana na msukumo wa kuiweka sawa thamani ya sarafu husika katika matumizi kulingana na mwenendo wa kiuchumi kutokana na athari ya mfumuko wa bei ambao ni jambo la kiasili katika mfumo wa sarafu kidunia, ambapo baada ya muda, nguvu ya kimanunuzi ya kiasi cha fedha (currency denomination) itapungua kutokana na kuongezeka mfumuko wa bei.
Katika wakati wa hali mbaya kiuchumi iliyokithiri, kama ilivyowahi kutokea katika nchi nyingine, mabadiliko ya sarafu yanaweza kuja kwa sura ya kuacha kabisa mfumo wa sarafu fulani na kulazimika kutumia mfumo wa nchi nyingine (currency substitution).
Hii si ishara nzuri itakapofikia, kwa sababu inaashiria nchi ipo katika mgogoro mkubwa pengine kiuchumi, machafuko, au sababu za kimfumo wa fedha kama kutokea mfumuko wa bei wa kupita kiasi (hyperinflation).
Kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kutoa elimu ya fedha na kuongeza matumizi ya teknolojia ya fedha katika kuhifadhi, kufanya, na kupokea miamala ya malipo. Hii itasaidia kupunguza kiwango cha sarafu na matumizi ya fedha taslimu kilichoko katika mzunguko.
Kwani kadiri watu wengi wanavyotumia fedha taslimu, ndivyo inavyoongeza gharama za uchapishaji na kuingiza fedha mpya, pamoja na hatari ya ulaghai wa noti feki na changamoto nyingine. Kuhamia katika uchumi wa fedha kidijitali kutasaidia kupunguza changamoto hizi na kuimarisha mifumo ya kifedha.