Mikakati ya Serikali kuipa nguvu ATCL

Dodoma. Serikali imesema miongoni mwa miradi mikubwa ya maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 itakayopewa kipaumbele,  ni pamoja na ufufuaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Mei 6, 2024 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Wizara hiyo imeliomba Bunge kuidhinisha Sh2.7 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na uekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo Sh114.7 bilioni ni kwa matumizi ya kawaida na Sh2.6 trilioni ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imeendelea kufanya biashara ya usafiri wa anga kwa kusafirisha abiria na mizigo ndani na nje ya Tanzania ili kuinua uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi.

“Aidha, ATCL imeanza hatua kwa hatua kujihudumia katika baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na matengenezo ya ndege, utoaji wa huduma uwanjani (ground handling services) kwa kituo cha Dodoma na huduma ndani ya ndege pamoja na kutoa huduma ya mafunzo kwa wahudumu wa ndani ya ndege kupitia chuo chake cha ATCL Training Centre,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) katika sehemu ya 5.7 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 Ibara ya 59 (i) ilidhamiria kuendelea kufufua ATCL kwa kununua ndege ili kuimarisha ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

“Nichukue fursa hii kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa, Serikali imeendelea kuboresha utendaji wa ATCL kwa kununua ndege mpya na kuboresha miundombinu wezeshi ya kutolea huduma ikiwa ni pamoja na majengo na karakana.

“Uboreshaji wa ATCL unalenga kuongeza ufanisi wa utendaji ili kuweza kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi la kusafirisha mizigo na abiria; na kuchagiza shughuli za utalii, kilimo ikiwa ni pamoja na kusafirisha mazao yanayoharibika haraka  na madini,” amesema.

Amesema ununuzi wa ndege na uboreshaji wa miundombinu umelenga kuipunguzia ATCL gharama za uendeshaji na kuifanya iwe shindani katika soko la usafiri wa anga duniani.

Profesa Mbarawa amesema uboreshaji wa  ATCL umeongeza utendaji ambapo  hadi kufikia Machi, 2024, imeendelea kutoa na kuboresha huduma za usafiri wa anga kwa kusafirisha abiria na mizigo ndani na  nje ya Tanzania.

“Kwa takwimu zilizopo, ATCL ilisafirisha abiria 850,660 ikilinganishwa na abiria 826,594 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 2.91.

“Kati ya abiria waliosafirishwa, abiria 650,221 walikuwa ni wa ndani ya nchi na abiria 200,439 walikuwa ni wa nje ya nchi,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Machi 2024, ATCL iliweza kusafirisha jumla ya tani 5,034.2 za mizigo ndani na nje ya nchi ikilinganishwa na tani 2,680.9 zilizosafirishwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 87.78.

“Ongezeko hilo limetokana na kuanza kufanya kazi kwa ndege  ya mizigo aina ya Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54 ambayo husafirisha mizigo kati ya Dar es Salaam na vituo vya Nairobi (Kenya) na Dubai mara moja kwa wiki, pamoja na vituo vingine ambavyo wateja wenye mizigo hukodi vikiwemo vya Mumbai (India), Eldoret (Kenya), Mombasa (Kenya), Bujumbura (Burundi).

“Kinshasa (Kongo DRC), Bangui (Afrika ya Kati), N’Djamena (Chad), Entebbe (Uganda), na Lusaka (Zambia). Ndege hii imesafirisha tani 2,084.7 za mizigo sawa na asilimia 41.41 ya mizigo iliyosafirishwa katika kipindi tajwa,” amesema.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake leo bungeni jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Amesema katika kuendelea kuongeza wigo wa huduma zake, ATCL imeendelea kutoa huduma ya usafiri wa anga katika vituo 24 ambapo vituo 13 ni vya ndani ya nchi na vituo 11 ni vya nje ya nchi.

Profesa Mbarawa amesema vituo vya ndani ya nchi ni Arusha, Bukoba, Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Kilimanjaro, Kigoma, Songwe, Mpanda, Mwanza, Songea, Tabora na Zanzibar. Vituo vya nje ya nchi ni Bujumbura, Dubai, Entebbe, Hahaya, Guangzhou, Harare, Lubumbashi, Lusaka, Mumbai, Nairobi na Ndola.

Amesema usimamizi na ununuzi wa ndege, kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi kufikia Machi 2024, Serikali ilikamilisha malipo ya ndege tatu  ambazo ni Boeing 737-9 Max mbili na Boeing 787-8 Dreamliner moja.

Profesa Mbarawa amesema ndege mbili aina ya Boeing 737-9 Max tayari zimewasili nchini ambapo ndege moja  ilipokelewa Oktoba 3, 2023 na nyingine Machi 26, 2024.

“Boeing 787-8 Dreamliner iliyosalia inatarajiwa kuwasili mwishoni mwa  Mei, 2024. Kuwasili kwa ndege hiyo kutaifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 16.

“Ndege hizo zitasaidia ATCL kuendelea kupanua mtandao wake wa safari za ndani na nje ya nchi ili kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi kama utalii, madini, biashara, kilimo, mifugo na uvuvi,” amesema.

Profesa Mbarawa amesema katika kipindi husika, ATCL ilinunua vifaa na vipuri kwa ajili ya kuwezesha kufanya matengenezo makubwa na madogo ya ndege aina zote yaliyoruhusiwa katika karakana zilizopo katika kiwanja cha JNIA na KIA.

Amesema ukarabati wa  miundombinu katika karakana ya kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), (KIMAFA) na JNIA  unaendelea.

“Pia, ukarabati wa nyumba 38 zilizopo KIA unaendelea na utekelezaji wake umefikia asilimia 47. Ukarabati wa nyumba hizi ni muhimu kwa ajili ya matumizi ya watumishi wa ATCL wataokuwa wakitoa huduma katika kituo cha KIA.

“Kituo cha KIA ni kituo muhimu kwa ajili ya utalii hivyo ATCL itafanya kituo hicho kuwa kitovu kidogo (sub hub) kadri utoaji wa huduma unavyokuwa.

“Serikali pia imeiwezesha ATCL kuanza ujenzi wa karakana mpya yenye uwezo wa kuhudumia ndege kubwa na kuifanya JNIA kitovu cha safari za ATCL, ujenzi wa Ofisi za ATCL – Dodoma ili kuhakikisha utoaji huduma Makao Makuu ya

Nchi unakuwa wa haraka. Pia, Serikali imeendelea na ulipaji wa madeni ya zamani ya ATCL,” amesema.

Amesema Sh18.58 bilioni zimelipwa kwa wastaafu ikiwa ni sehemu ya madeni yaliyorithiwa na ATCL kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mpango wa ufufuaji.

“Hadi sasa madeni kiasi cha Sh148.95 bilioni sawa na asilimia 64 tayari yamelipwa na kubakia kiasi cha Sh82 bilioni sawa na asilimia 36,” amesema.

Amesema Serikali kupitia ATCL imeendelea kuajiri watumishi ambapo hadi kufikia Machi 2024, ATCL ilikuwa na watumishi 792 ikilinganishwa na watumishi 689 waliokuwepo katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2022/23.

Kamati yapongeza uendeshaji ACT

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Miundombinu, Moshi Kakoso akisoma maoni ya kamati amesema kuhusu uendeshaji wa ATCL, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kununua ndege za abiria na mizigo.

“Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Kamati inaishauri Serikali kubuni njia bora zaidi zitakazoongeza ufanisi wa uendeshaji wa ATCL ili shirika hilo liboreshe huduma zake kwa wasafiri, kujiendesha, kuzalisha faida na hatimaye kuongeza pato la Serikali,” amesema.

Related Posts