Unguja. Kaimu Kiongozi wa Timu ya Kazi kutoka Benki ya Dunia, Lulu Dunia amemtaka Mkandarasi wa mradi wa uimarisha Miji Unguja (AUP-U), kuuwekea mpango kazi na muda wake ili kujipima katika kuukamilisha.
Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkuu wa Ukuzaji Uchumi Jumuishi Zanzibar (BIG-Z) unaogharimu Dola za Marekani 150 (Sh404.472 bilioni unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Juni 2021 hadi Juni 2026.
Akizungumza baada ya timu hiyo kutoka benki ya dunia kutembelea mradi huo, Lulu amesema hii ni kutokana na ujio wa tathmini ya kati ya mradi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
“Ni vyema kila kitu kupangwa ndani ya muda kabla ya kufika tarehe za kumalizika kwa mradi wa BIG-Z Juni, 2026 pamoja na kuzungumzia masuala ya usalama wa kimazingira ikiwemo ujenzi wa vyoo hasa katika eneo jipya la Ofisi za mkandarasi na mshauri elekezi,” amesema.
Kwa upande wake Mhandisi Mussa Natty, amemtaka mshauri elekezi kuisaidia timu ya usimamizi wa mradi (PMT), kuhakikisha mkandarasi anatumia vifaa vilivyoingizwa kwa utekelezaji wa mradi huo ili kusaidia kuondoa changamoto ya kuzorota kwa utekelezaji wa miradi na kupoteza ubora uliokusudiwa.
Pia, amesema ni muhimu kuwasimamia wananchi wote waliolipwa fidia kubomoa kulingana na fidia zao walizolipwa.
‘’ Hii inaonesha kuwa baadhi ya waathirika wa miradi ya uimarishaji miji Unguja (AUP-U) kubomoa nyumba kinyume na alama walizowekewa,’’ amesema.
Naye mshauri elekezi, Dar Al Handasah, ameahidi kumsimamia mkandarasi (CRJE East Africa) kikamilifu ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa miradi kama ilivyokusudiwa.
Amesema changamoto kubwa ilikuwa ni upatikanaji wa vifaa na wafanyakazi lakini limeshatatuliwa, hivyo atahakikisha anafanya kazi kazi kwa bidii na kumaliza kwa wakati uliopangwa.
Ziara hiyo ilijumuisha timu ya watendaji kutoka Benki ya Dunia, timu ya usimamizi wa mradi (PMT) na wadau mbalimbali wa Mradi wa Uimarishaji Miji Unguja, waliotembelea maeneo yaliyoanza utekelezaji wa miradi ikiwemo barabara ya Gongostoo – kwa Mpechi – kwa Najim, barabara ya Jang’ombe (Kwa Mchina Mataa hadi Magereza) na sehemu ya utekelezaji wa mtaro mkubwa wa Shimo la Nguruwe Meya.