Ditram Nchimbi ajipa muda Biashara United

MSHAMBULIAJI wa Biashara United, Ditram Nchimbi amesema bado ni mapema kuikatia tamaa timu hiyo kwenye mbio za kupanda Ligi Kuu Bara huku akijipa muda katika kufunga mabao na kutwaa kiatu cha ufungaji bora kwenye Ligi ya Championship.

Nchimbi aliyejiunga na Biashara ya Mara msimu huu baada ya kupumzika kucheza soka kwa msimu mmoja, ameshafunga bao moja kwenye Championship dhidi ya Mbeya Kwanza mchezo wa sare ya 1-1 katika Uwanja wa Karume, Musoma.

Biashara inakamata nafasi ya 12 ikiwa na pointi nane katika michezo saba, imeshinda miwili, sare mbili na kupoteza mitatu huku ikifunga mabao manne na kuruhusu sita.

Nchimbi aliliambia Mwanaspoti uwepo wa wachezaji wengi kwenye michuano hiyo kutoka Ligi Kuu huku timu nyingi zikiwa imara, ndiko kunafanya kuwa ngumu na upinzani mkali huku timu zikipata ugumu kushinda kirahisi.

“Hakuna changamoto inayotufanya kupoteza mechi zetu, yaani unakuta sisi tumejiandaa na wenzetu wanajiandaa zaidi labda au inatokea tu kuna muda upepo unakuwa haukai vizuri tu inategemea tu na maandalizi ya hizo mechi,” alisema Nchimbi.

“Kwa hiyo mimi naamini hapa katikati kuna kaupepo tu kamepita siku mbili tatu ka matokeo mabovu lakini tutakuwa vizuri tu. Kikubwa ambacho mashabiki wetu wanatakiwa wajue mambo yanapokuwa magumu wanatakiwa kuongeza mshikamano watusapoti asilimia 100 tufanye vizuri,” alisema.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, Polisi Tanzania na Mwadui alisema utimamu wake wa mwili umerejea kwa asilimia 100 na yuko tayari kupambana na kuisaidia timu hiyo huku akijipa mtihani wa kupachika mabao na kukidhi kiu ya mashabiki wake.

“Nimepata mechi nyingi za kucheza naamini nimeshakuwa sawa asilimia 100, nacheza nafasi ambayo watu wanategemea nifunge kwahiyo hiyo ni changamoto ambayo nimejipa mwenyewe. Mechi bado ni nyingi nitafunga tu na kusogea sehemu ninayoitaka,” alisema Nchimbi.

Related Posts