Dodoma. Mbunge wa Mbongwe (CCM), Nicodemas Maganga amehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha wanasiasa wanalindwa kikamilifu na kuhakikisha wanamaliza maandamano na mikutano yao salama wakati wa uchaguzi.
Akiuliza maswali ya nyongeza bungeni Alhamisi Novemba 7, 2024, Maganga amesema mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi na katika sheria za Tanzania maandamano na mikutano ni vitu vinaruhusiwa.
“Zinapoanza kampeni, je mmejipangaje kuhakikisha kuwa wanasiasa tunalindwa kikamilifu na kuhakikisha tunamaliza mikutano salama na maandamano yetu,” amehoji Maganga.
Pia amesema Tanzania imekuwa na matukio ya wananchi kuchonganishwa hasa na Jeshi la Polisi lakini ukweli ni kwamba wanaofanya matukio ni watu wengine wakitumia mgongo wa Jeshi la Polisi.
Amehoji ni ipi kauli ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya kuhakikisha wanawalinda polisi na kuondoa utapeli unaofanywa na watu waovu.
Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge, Musa Zungu alikataa swali hilo kujibiwa huku akitoa sababu ya kufanya hivyo ni kutokuwa katika swali la msingi la mbunge huyo.
“Mheshimiwa Maganga swali la pili halitalijibiwa kwa sababu halipo kwenye swali la msingi, mhesmiwa Waziri endelea”amesema Zungu.
Akijibu swali la kwanza la nyongeza, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo amesema Tanzania inaongozwa kwa mujibu sheria na utaratibu.
“Kwa hiyo kama kuna watu ambao wanaofanya fujo ama kuchonganisha Jeshi la Polisi. Naomba nitoe wito kwa watu hao waache mara moja na watakaobainika sheria itachukua mkondo wake ikiwemo kufikishwa mahakamani,” amesema.
Katika swali la msingi, Maganga amehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha raia wa kigeni hawashiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Akijibu swali hilo, Sillo amesema raia wa Tanzania ndio wenye haki ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi kuu kwa kupiga kura au kuchaguliwa kuwa viongozi kwa mujibu wa sheria.
Amezitaja sheria hizo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya Mwaka 2024 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 na kanuni zake za mwaka 2024.
“Katika kusimamia vipindi vyote wakati wa uchaguzi, Serikali imekuwa ikitoa elimu ya uraia kwa watendaji (waandikishaji na wasimamizi wa uchaguzi) ili kuhakikisha raia wa Tanzania wenye sifa ndio wanaoshiriki katika chaguzi na sio raia wa kigeni,”amesema.
Aidha, amesema inapobainika kwamba kuna mtu anadiriki kujiandikisha ama kutafuta fursa ya kugombea na zipo taarifa au tuhuma, kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi, mhusika huyo huwekewa pingamizi.
Amesema na ikithibitika mtu huyo huchukuliwa hatua za kisheria ikiwepo kuondolewa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura sanjari na kufikishwa mahakamani.