Jukwaa la Wahariri Tanzania latema nyongo, lamshukia Waziri Silaa

Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeeleza kusikitishwa kwake na mwenendo wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kutohudhuria matukio muhimu ya kihabari anayoalikwa kama mgeni rasmi.

Miongoni mwa matukio hayo ni la Mkutano Mkuu wa TEF unaofanyika leo Alhamisi, Novemba 7, 2024 jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Silaa alialikwa kuwa mgeni rasmi, lakini ametumwa mwakilishi.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile amesema TEF inasikitishwa kusuasua kuhudhuria matukio hayo ikiwemo Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) zilizotolewa Septemba 28, 2024.

Balile ameyasema hayo katika mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo ‘Weledi kwa Uhimilivu wa Vyombo vya Habari,” ambapo Waziri Silaa amemtuma Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa.

“Hajaonekana katika matukio mengine ya Jumuiya wa Maofisa Uhusiano PRST jijini Arusha. Tukasikia aliitwa Mbeya hakwenda na Mkutano wa nane Wahariri unaoendelea tunakuomba Naibu Katibu Mkuu kumfikishia salamu za kusikitishwa kwetu,” amesema Balile.

Amesema mwenendo huo haufurahishi na ameomba kukaa na tasnia ya vyombo vya habari kuweza kufahamu yaliyomo ikiwemo tabia na mienendo yao.

Huku wahariri wakashangilia, Balile amesema, Waziri Silaa anapaswa kutambua tasnia ya habari ni sehemu ya wadau wake muhimu anaopaswa kushirikiana naye kwa ukaribu.

Hata hivyo, TEF imemshukuru Waziri huyo kwa kuteua bodi ya ithibati inayokwenda kuleta utekelezaji wa sheria ya huduma za habari hatua aliyoichukua baada ya kuingia madarakani.

Mbali na masikitiko hayo Balile amesema zipo baadhi ya taasisi na mashirika yasiyotoa ushirikiano ipasavyo katika vyombo vya habari jambo ambalo linakwamisha mchakato wa maendeleo.

Lilimesema ushirikiano kati ya vyombo vya habari na taasisi na mashirika ya umma katika utoaji wa taarifa ni jambo linalochochea maendeleo kwenye tasnia hiyo muhimu.

Jukwaa hilo limesema ushirikiano unapotolewa pale vyombo vinapohitaji taarifa unasaidia lakini ikiwa kinyume na hapo inakwamisha mchakato wa kuujulisha umma habari muhimu.

“Bado wapo wachache ambao hawataki kutoa taarifa hata ukiwaendea naomba Naibu Katibu Mkuu utusaidie uwafikishie salamu,” amesema Balile.

Amesema hata hatua ya Msajili wa Hazina kutaka mashirika na taasisi za umma kukutana na vyombo vya habari kuulizana maswali umesaidia kuongeza uaminifu kati yao ingawa wapo hao baadhi wasiotoa ushirikiano.

Akizitaja changamoto nyingine zinazowakabili ameitaja sheria ya mwaka 2016 ya Huduma za Habari iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 akisema kuna baadhi ya mambo yanapaswa kurekebishwa.

“Changamoto nyingine ni sheria inayomzuia mwekezaji kutoka nje ya nchi kumiliki zaidi ya asilimia 49 ya hisa katika kampuni ya habari kwani suala hilo linafifisha uchumi wa vyombo vya habari nchini,” amebainisha Balile.

Amesema hata mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ni makubwa ikiwemo kuwa mlalamikaji, muendesha mashtaka mtoa hukumu msimamizi wa utekelezaji wa hukumu.

Aidha, amepongeza Serikali kwa usimamizi bora uliopelekea Tanzania kupanda katika uhuru wa vyombo vya habari duniani hadi kufikia hadi 97 kutoka nafasi ya 143 katika uhuru wa vyombo vya habari duniani.

“Suala hili halijaja bure bali linatokana na uamuzi na usimamizi thabiti na maelekezo mahususi ya Rais Samia Suluhu Hassan uliopunguza maonyo na kukoromeana koromeana,” amesema.

Hata hivyo, akizungumza kwa niaba ya Waziri Silaa kwenye mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu, Mkapa ameahidi kufikisha salamu hizo za TEF huku akisema kutokana na sababu zilizonje ya uwezo wake ameshindwa kuhudhuria mkutano huo.

Mwananchi limemtafuta Waziri Silaa kwa simu ya mkononi ambapo simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Akijibu changamoto zingine zilizowasilishwa na TEF, Mkapa suala la umiliki wa wawekezaji wa kigeni ni la kisera na mchakato umeanza huku akiahidi kuwashirikisha. Amesema wanaendelea kupitia sera ili kuweka mfumo mzuri katika sekta ya habari.

“Tutaendelea kuwashirikisha katika michakato pia, wizara inaendelea kufanyia kazi ripoti ya hali ya uchumi wa vyombo vya habari nchini,” amesema Mkapa.

Baada ya ufunguzi kumalizika na mada mbalimbali kutolewa, suala hilo limeibuka tena kwa mmoja wa wahariri kutoa hoja akitaka maelezo ya Mwenyekiti wa TEF, Balile juu ya Waziri Silaa hoja hiyo ijadiliwe kwa kina.

Licha ya wahariri wengi kuiunga mkono lakini haikujadiliwa kwa maelezo kwamba wampe muda Waziri Silaa salamu zimfikie kupitia kwa Mkapa aliyepewa na au itajadiliwa siku zijazo za mkutano huo utakaomalizika Jumamosi, Novemba 9, 2024.

Katika hotuba yake, Mkapa ametoa rai katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea uchaguzi vyombo kuzingatia mambo muhimu ya weledi katika uandishi.

“Wahariri na waandishi wa habari mnaowajibu wa kudumisha amani kupitia kalamu na sauti zenu. Vilevile mnapaswa kuonesha Watanzania maendeleo yanayofikiwa na Serikali ikiwemo reli ya kisasa ya SGR na bwawa la umeme la Julius Nyerere,” amesisitiza.

Awali mkutano huo uliohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema jambo la kuzingatia kwa vyombo vya habari ni ukweli na haki ili kuilinda amani.

“Amani inakuja pale tunaporipoti kwa haki na usawa tunaposhika kalamu zetu, tuzingatie maadili katika kazi zetu za uandishi wa habari,” amesisitiza Mpogolo ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dae es Salaam.

Related Posts