Wazee miaka 60 kupamba bonanza la michezo MZRH

HOSPITALI ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) imeandaa bonanza la michezo mbalimbali itakayopambwa na wazee wenye umri wa miaka 60  kufukuza kuku na kuvuta kamba.

Bonanza hilo linatarajiwa kufanyika Novemba 9 mwaka huu kwenye Viwanja vya Chuo cha Uhasibu (TIA) ikiwa ni kuadhimisha wiki ya upimaji wa  magonjwa yasiyoambukizwa.

Katibu wa mashindano hayo, Joyce Komba ameyasema hayo alipozungumza na Mwanaspoti akibainisha kwamba maandalizi yamefikia asilimia 90.

Joyce amesema kupitia bonanza hilo kutakuwa na washiriki  kutoka taasisi mbalimbali, wadau wa michezo sambamba na kuibua vipaji kwa wasanii wachanga watakaoshiriki.

“Miongoni mwa michezo ni kufukuza kuku kwa wazee wenye zaidi ya miaka 60, kuvuta kamba, mpira wa miguu, mpira wa pete na mingine mingi sambamba na upimaji wa afya na uchangiaji wa damu,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hosptali ya Rufaa Kanda, Dokta Godlove Mbwanji amesema lengo la bonanza hilo ni kuikumbisha jamii kufanya mazoezi na kupima afya ili kukabiliana na magonjwa  hususani shinikizo la damu, tezi dume, kisukari, macho, figo, homa ya ini na mengineyo.

Dokta Mbwaji amesema zaidi ya wataalamu wa afya 1,200 watashiriki huku akitumia fursa hiyo kuitaka jamii kujitokeza kwa wingi kwa kutambua michezo ni afya.

Amesema kwa miaka ya sasa kuna changamoto kubwa ya kiafya kwa jamii inayochangiwa na kutofanya mazoezi na mifumo ya ulaji.

“Lengo la bonanza hili ni kuikumbusha jamii kuwa na mwamko wa kufanya mazoezi na ndiyo sababu kama hospitali wameona waje na mashindano mbalimbali ya michezo ambayo itasaidia kupunguza wahanga,” amesema Dokta Mbwanji.

Related Posts