KOCHA Mkuu wa Pamba, Fredy Felix ‘Minziro’, amesema baada ya timu hiyo kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu wa mabao 3-1, dhidi ya Fountain Gate Novemba 5, kwa sasa kikosi hicho kitakuwa na siku 14 za kufanyia marekebisho.
Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu, ilipata ushindi huo wa kwanza baada ya kucheza michezo yake tisa mfululizo jambo lililowafanya mabosi wa kikosi hicho kumfuta kazi aliyekuwa kocha Mserbia, Goran Kopunovic Oktoba 16, mwaka huu.
Akizungumza na Mwanaspoti Minziro alisema ushindi huo kwao umeamsha morali ya wachezaji baada ya kusota kwa muda mrefu, ingawa licha ya hayo ila ana kazi kubwa ya kufanya ya kuhakikisha anatengeneza mizani eneo la ulinzi na ushambuliaji.
“Kipindi hiki kimetoa nafasi kwetu kama benchi la ufundi kuangalia maeneo muhimu ya kuboresha kabla hatujarejea tena katika michezo ya ushindani, uwiano wa kufunga na kuruhusu mabao sio mzuri hivyo tunafanyia kazi suala hilo kwa haraka.”
Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za Geita Gold na Maafande wa Tanzania Prisons, aliongeza, baada ya mchezo wao wa Novemba 21 dhidi ya Simba kuondolewa, utawapa nafasi nzuri ya kupambana na changamoto iliyopo.
“Bado hatupo sehemu salama kwa sababu kama unavyoona pia kuna ushindani mkubwa na kila timu imejipanga vizuri, tutapambana zaidi ili kutoka chini tulipo, kufanikisha hilo ni lazima pia tujue namna nzuri ya kutatua mapungufu tuliyokuwa nayo.”
Tangu Minziro ajiunge na kikosi hicho Oktoba 17, mwaka huu akichukua nafasi ya Goran Kopunovic, huo ulikuwa pia ushindi wake wa kwanza baada ya kuanza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Kagera Sugar na kuchapwa bao 1-0 na Tabora United na Namungo FC.
Pamba iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, imeanza msimu huu vibaya tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita wakati inashiriki Ligi ya Championship ambapo ilipomaliza nafasi ya pili.
Msimu uliopita timu hiyo katika michezo 30 iliyocheza ilishinda 20, sare saba na kupoteza mitatu ikiwa imekusanya pointi zake 67.