Unguja. Awamu ya nne ya tuzo kupitia mradi wa kuwajengea wanawake uwezo katika uongozi (SWIL), limezinduliwa huku vyombo vya habari na waandishi wa habari wakikaribishwa kushiriki katika tuzo hizo ziwe ushahidi wa nguvu ya uandishi wa habari katika kuleta mabadiliko chanya.
Tuzo hizo za uwiano wa kijinsia kwa vyombo vya habari, zinatolewa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (Tamwa Zanzibar) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (Juwaza), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela) na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (Pegao) chini udhamini wa Norway.
Akizungumza kuhusu ufunguzi wa pazia hilo, Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar, Dk Mzuri Issa leo Novemba 7, 2024 amesema kupitia tuzo hii, Tamwa ZNZ inalenga kuhamasisha vyombo vya habari na waandishi wa habari kuunga mkono sauti za wanawake.
“Tunawakaribisha waandishi wa habari na vyombo vya habari kushiriki katika tuzo hizi muhimu, ili habari zenu ziwe ushahidi wa nguvu ya uandishi wa habari katika kuleta mabadiliko chanya,” amesema.
Mbali na kuunga mkono sauti za wanawake na kukuza uandishi wa habari wenye kuzingatia usawa wa kijinsia ili kuchangia mabadiliko ya kijamii kwa kuonesha nafasi za wanawake na uwezo wao katika uongozi ili kuleta maendeleo.
Tuzo hiyo yenye ujumbe unaosema ‘kalamu yangu, mchango wangu kwa Wanawake’ itatambua vyombo vya habari na waandishi wa habari Zanzibar vinavyoandika habari za kina kuhusu mafanikio, changamoto, michango ya wanawake katika uongozi, na vinavyoshiriki kikamilifu katika kukuza usawa wa kijinsia kupitia kazi zao.
“Mara hii tuzo hizi zinalenga zaidi kutambua vyombo vya habari vyenye mtiririko mzuri wa kusaidia kuongeza wanawake katika nafasi za uongozi. Hivyo vigezo vitakavyotumika ni kuwa na sera ya kijinsia, dawati la kijinsia, zana za tathmini na ufuatiliaji wa masuala ya usawa wa kijinsia,” amesema
Nyingine ni idadi ya habari zilizoandikwa kuhusu wanawake na uongozi na nafasi ya wanawake waandishi wa habari katika chombo cha habari.
Amesema mradi wa SWIL uliwahi kuwapa mafunzo vyombo vya habari 11 kutoka Unguja na Pemba kuandika na kuweka kumbukumbu na kufanya ufuatiliaji na tathmini katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2023.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, tuzo hizo zitakuwa uandishi wa habari za makala katika magazeti, uandishi wa habari wa vipindi katika redio, televisheni na uandishi wa habari wa makala katika mitandao ya kijamii kuanzia Januari Mosi hadi Desemba 31, 2024.
Amesema kama ilivyokuwa kwenye vyombo vya habari SWIL pia ilikaa na waandishi wa habari 170 kwa mafunzo na majadiliano kuhusu kuandika habari nzuri za wanawake na uongozi.
Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano Tamwa Zanzibar, Sophia Ngalapi amesema; “Ni wakati sasa waandishi kuchangamkia fursa hii, kwani inachochea uandishi wenye tija na kukuza uwezo wa mmojammoja na kupanua wigo wa kungamua mambo.”