EWURA YAHAKIKI TAARIFA ZA MAMLAKA ZA MAJI 82 NCHINI

Mkurugenzi wa Gesi Asilia EWURA, Mha. Poline Msuya, akizungumza na watendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, wakati wa kikao kazi cha kuhakiki taarifa za utendaji za mamlaka hizo kilichofanyika Ofisi za EWURA makao makuu jijini Dodoma.

……..

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imefanikisha uhakiki wa taarifa za utendaji wa Mamlaka 82 za Maji na Usafi wa Mazingira nchini,ili kupata takwimu sahihi zitakazotumika kwenye Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka hizo kwa mwaka 2023/24.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mha. Poline Msuya, akihitimisha kikao kazi cha watendaji wa mamlaka za maji, Novemba 6, jinini Dodoma, , amesema EWURA imehakiki takwimu hizo kupitia mfumo ulioboreshwa wa MajIS, ambao ni mahsusi kwa ajili ya kukusanya na kuhifadhi taarifa za utendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini.

“Leo tumefanikisha zoezi hili kwa ufanisi na umakini mkubwa. Natoa rai kwa watendaji wote wa mamlaka za maji kujiridhisha na kuzitambua takwimu zote zilizowekwa kwenye mfumo,” alisema.

Taarifa zilizohakikiwa ni za kiwango cha maji yanayozalishwa, hali ya ufungaji wa dira za maji, muda na hali ya upatikanaji wa huduma kwa kuzingatia wastani wa idadi ya maunganisho ya maji, takwimu za usafi wa mazingira na ubora wa maji, mahitaji ya maji, takwimu za makusanyo ya maduhuli na tathmini ya viashiria/maeneo vinavyosababisha upotevu wa maji.

Mha. Wilfred Marko Gichogo, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, aliwasisitiza watendaji hao kuhakikisha kila wakati wanawasilisha takwimu kwenye mfumo kwa wakati na kwa usahihi.

Watendaji kutoka Mamlaka za maji za mikoa, miradi ya kitaifa, wilaya na miji midogo pamoja na wawakilishi kutoka Wizara za Maji na Afya wameshiriki kikao kazi hicho kilichoandaliwa na EWURA, ili kuhakiki na kuthibitisha taarifa za utendaji wao kwa lengo la kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi za utendaji wa sekta ya maji nchini.

Mkurugenzi wa Gesi Asilia EWURA, Mha. Poline Msuya, akizungumza na watendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, wakati wa kikao kazi cha kuhakiki taarifa za utendaji za mamlaka hizo kilichofanyika Ofisi za EWURA makao makuu jijini Dodoma.

Wakurugenzi na Watendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini wakieendelea na zoezi la uhakiki wa taarifa za utendaji kupitia mfumo wa MaJIS wakati wa kikao kazi, Ofisi za EWURA makao makuu, jijini Dodoma, Novemba 6, 2024.

Picha ya pamoja ya Wakurugenzi wa Watendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira wakati wa kikao kazi cha kuhakiki taarifa za utendaji kilichanyika katika Ofisi za EWURA Makao Makuu, jijini Dodoma. Walioketi, katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu EWURA, Mha. Poline Msuya, kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira EWURA, Mha. Genzabuke Madebo na kushoto ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mha. Wilfred Gichogo.

Related Posts