Dar es Salaam. Uamuzi wa kupewa dhamana au kutopewa dhamana dhidi ya mshtakiwa, Ferdnand Ndikuriyo (27) maarufu Chuma cha Chuma, unatarajia kusikilizwa Novemba 20, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Ndikuriyo ambaye ni msanii wa muziki na raia wa Burundi anakabiliwa na shtaka moja la kuwepo nchini bila kuwa na kibali.
Mshtakiwa huyo mwenye makazi yake ya muda, Mbezi Louis, Dar es Salaam alifikishwa Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya jinai namba 31005/2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Ushindi Swallo.
Baada ya kusomewa shtaka hilo siku hiyo, alikana na upande wa mashtaka uliwasilisha maombi mahakamani hapo ya kuzuia dhamana dhidi ya mshtakiwa, kutokana na sababu za kiusalama.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo aliomba apewe dhamana kwani ana mtoto mdogo ambaye anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo hadi leo Alhamisi, Novemba 7, 2024 kwa ajili ya kusikiliza maombi hayo yaliyowasilishwa na Serikali pamoja na kutoa uamuzi.
Hata hivyo, leo shauri hilo liliitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa maombi ya kuzuia dhamana lakini hakimu anayesikiliza kesi hiyo Ushindi Swallo, yupo likizo.
Wakili wa Serikali Grace Nyarata akisaidina na Ezekiel Kibona akishirikiana alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga kuwa shauri hilo liliitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa maombi ya kuzuia dhamana ya upande wa mashtaka, lakini hakimu anayesikiliza shauri hilo ameanza likizo.
“Kutokana na hali hii, tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na kesi,” amedai Wakili Nyarata.
Wakili Kibona ameongezea tayari upande wa mashtaka umeshasajili maombi hayo kwa njia ya mtandano na kwamba wanasubiri kujua yamepangiwa hakimu nani wa kuyasikiliza.
Kibona baada ya kueleza hayo, mshtakiwa aliikumbusha mahakama izingatie ombi lake kwa kuwa yeye ndio anayetegemewa na familia yake.
Hakimu Ruboroga baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, alisema hawezi kusikikiza shauri hilo wala kutoa uamuzi kutokana na shauri hilo kuwa la Hakimu mwingine, ambaye yupo likizo.
“Kwa kuwa kesi hii sio yangu, siwezi kutoa maamuzi wowote, ila niwashauri muende kwa Hakimu Mfawidhi ili yeye aweze kuamua anampangia hakimu nani aweze kusikiliza maombi haya,” alisema Hakimu Ruboroga.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Ruboroga aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 20, 2024 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na kuzuiliwa dhamana.
Katika kesi ya msingi, Chuma anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 18, 2024 eneo la Upanga, Las Vegas Casino, Ilala, Dar es Salaam.
Ilidaiwa kuwa, mshitakiwa akiwa eneo hilo, alibainika kuwepo nchini bila kuwa na kibali, wakati akijua kuwa ni kinyume cha sheria.