Vyama vya upinzani vya Ujerumani na makundi ya wafanyabiashara wamemhimiza Kansela Olaf Scholz kuitisha uchaguzi mpya haraka. Scholz alimtimua Waziri wa Fedha Christian Lindner wa chama kinachounga mkono sera za kibiashara cha Free Democratic – FDP. Hatua hiyo ilimlazimu Lindner ambaye amekuwa akitofautiana wazi wazi na Scholz kuhusu sera za kiuchumi, kukiondoa chama cha FDP katika serikali ya muungano ya pande tatu na Social Democratic – SPD chake Scholz na chama cha Kijani.
Soma pia: Serikali ya Ujerumani yasambaratika kutokana na uchumi unaoyumba
Baada ya kutimuliwa, Lindner amesema “Kitu sahihi cha kufanya kwa nchi yetu itakuwa ni kuitisha kura ya imani mara moja na kuandaa uchaguzi mpya. Katika demokrasia, hakuna anayepaswa kuwaogopa wapiga kura. Uchaguzi mpya mara baada ya kushindwa kwa serikali ya Scholz sio tu muhimu kwa demokrasia. Nchi yetu haina muda wa kupoteza.
Sasa Kansela Scholz amesema ataiongoza serikali ya wachache bungeni, licha ya miito kutoka kwa upinzani ya kuitisha uchaguzi wa mapema. Serikali hiyo itajumuisha chama cha Scholz cha SPD na cha Kijani hadi mapema mwakani. Hii ni hata baada ya kiongozi wa kundi kubwa la upinzani bungeni Friedrich Merz kutoka chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia Christian Democratic – CDU kutoa wito wa kura ya kutokuwa na imani na kisha uchaguzi mpya. Scholz amesisitiza tena leo kuwa hataki kuitisha kura ya imani kabla ya Januari 15.
Scholz na Merz, ambaye anatumai kumrithi kansela, walifanya leo mazungumzo mjini Berlin kwa karibu nusu saa. Walijadili uwezekano wa kupata tarehe ya uchaguzi ujao lakini Merz aliondoka bila kusema lolote.
Soma pia: Scholz aiweka rehani serikali kwa kumtimua waziri wa fedha
Rais Frank-Walter Steinmeier alimpa waziri aliyetimuliwa Lindner, na mawaziri wengine wawili wa FDP waliojiuzulu: Bettina Stark-Watzinger wa Elimu na Marco Buschmann wa sheria, vyeti vyao vya kuachishwa kazi.
Waziri wa Uchukuzi Volker Wissing, ambaye pia ni wa FDP amesema baada ya mazungumzo na Scholz, ameamua kusalia ofisini na badala yake kuondoka chamani. Scholz alimuomba aongeze wizara ya sheria kwenye majukumu yake.
Rais Steinmeier pia amemteuwa Jörg Kukies, mshauri wa kiuchumi wa Scholz, kuwa Waziri wa fedha. Waziri wa kilimo Cem Özdemir kutoka chama cha Kijani amekubali kuchukua wizara ya Elimu. Steinmeier amesema ni wakati wa uwajibikaji “Huu si wakati wa mbinu za kijanja na mikwaruzano. Ni wakati wa umakini na uwajibikaji. Natarajia kila mmoja awajibike. Natarajia wote walio katika nafasi za uwajibikaji wasimame kidete na kuzitatua changamoto zinazotukabili.”
Viongozi wa Ulaya wameonesha imani yao
Maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya hawajaonesha wasiwasi wowote kuhusiana na kuvunjika kwa serikali ya muungano wa Ujerumani na uwezekano wa kutishwa uchaguzi wa mapema katika nchi hiyo kubwa kiuchumi ambaye ni mwanachama wa umoja huo.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema kuwa uchaguzi ni kitu cha kawaida katika kila demokrasia. Amesema ni juu ya Ujerumani yenyewe kujadili namna ya kuutatua mzozo wa kisiasa mjini Berlin.
Rais wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola aliunga mkono kauli hiyo akisema Ujerumani ni mshirika muhimu katika Umoja wa Ulaya. Viola Amherd, rais wa Uswisi ambayo ni Jirani wa Ujerumani katika upande wa kusini amesema anaamini nchi hiyo itatatua matatizo yake haraka iwezekanavyo.
Ubelgiji, Finland, Norway pia zimeelezea matumaini yao zikisema ni muhimu kwa Ujerumani kuandaa uchaguzi mpya haraka.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami – NATO Mark Rutte amemuunga mkono Scholz kutimiza majukumu ya usalama wan chi yake licha ya kusambaratika kwa muungano tawala.
Afp, ap, dpa, reuters