Watafiti wapendekeza njia kumaliza migogoro ya rasilimali

Dar es Salaam. Kushirikisha kikamilifu jamii wenyeji katika kusimamia na kunufaika na rasilimali zilizopo maeneo yao, kunatajwa kuwa suluhisho la kudumu la utatuzi wa migogoro inayohusu matumizi ya maliasili nchini.

Hayo yameelezwa na watafiti katika mhadhara kwa umma uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ukiwa sehemu ya kongamano la kimataifa la nane la Sauti ya Sayansi ya Jamii lililoandaliwa na Chuo cha Sayansi ya Jamii (CoSS).

Kongamano hilo la siku tatu kuanzia Novemba 6 hadi 8, 2024 linanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Afrika katika nyakati za sintofahamu; matishio, ustahimilivu na mustakabali wa baadaye.’

Migogoro inayohusiana na rasilimali nchini hutokana na mgongano wa masilahi kati ya uhifadhi, maisha ya wenyeji, na maendeleo ya kiuchumi.

Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) na UDSM wanapendekeza mabadiliko ya mbinu inayohakikisha jamii zinahusishwa na zinanufaika na rasilimali hizo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira cha AKU, Dk Emmanuel Sulle, akitoa mhadhara leo Novemba 7, amesema migogoro inayohusu rasilimali ina mizizi ya kihistoria.

“Hili linatokana na enzi za ukoloni ambako kanuni zilibana ufikiaji wa wenyeji katika misitu, wanyamapori, na ardhi ya kilimo.

“Athari za sheria hizi bado zinahisiwa hadi leo, sera mara nyingi zinatoa kipaumbele kwa udhibiti wa Serikali juu ya haki za wenyeji hali inayosababisha migogoro ya mara kwa mara,” amesema.

Chanzo kikuu cha tatizo hilo kinahusishwa na sera za usimamizi wa ardhi ambazo licha ya mabadiliko, bado zinaipa Serikali Kuu mamlaka makubwa, mara nyingi kwa gharama ya ushiriki wa jamii.

Kwa mujibu wa Dk Sulle, ambaye pia ni Mkuu wa Kampasi ya AKU Arusha, juhudi za hivi karibuni za kuhusisha jamii katika uhifadhi zimeonyesha matumaini lakini hazitoshi.

“Kuwahusisha jamii katika uhifadhi kumeonekana kuwa na mafanikio katika maeneo kadhaa, lakini tunahitaji msaada wa sera pana kwa mabadiliko yenye maana,” amesema.

Mtaalamu mwandamizi, Profesa Issa Shivji amesema uhifadhi wa kweli hauwezi kufanikiwa bila ushiriki wa jamii za wenyeji.

“Miti, wanyamapori, na rasilimali zingine ziko katika hali yao ya sasa kwa kiasi kikubwa kutokana na jamii ambazo zimezihifadhi kabla ya juhudi za uhifadhi rasmi kuanza,” amesema na kuongeza:

“Hata hivyo, Tanzania, kama nchi nyingi, bado inafuata uhifadhi wa ngome (fortress conservation), ambao unawapuuza watu ambao wamekuwa walinzi wa rasilimali hizi kwa vizazi.”

Migogoro kama hiyo pia imeonekana kati ya wafugaji na wakulima, polisi na jamii katika maeneo ya madini, na maafisa wa wanyamapori na wakazi wa vijijini. Wataalamu wanakubaliana kuwa migogoro hiyo inachangiwa kwa kiasi fulani na ukosefu wa mawasiliano na elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa rasilimali.

Kihistoria, Tanzania imepiga hatua kwa kiasi Fulani katika kushirikisha jamii. Sera ya Wanyamapori ya mwaka 1998 ilianzisha masharti ya jamii kushiriki katika uhifadhi na kunufaika moja kwa moja na rasilimali zilizo ndani ya maeneo yao.

Hata hivyo, shinikizo la nje na ugumu wa sheria za ardhi umepunguza athari zake.

“Ingawa sheria za ardhi zinatoa nafasi ya kidemokrasia ya utawala wa ardhi, ambapo ridhaa ya jamii inahitajika, sera hizi mara nyingi huathiriwa na masilahi ya nje,” amesema Dk Sulle.

Wataalamu wanatoa wito wa kuimarisha majadiliano kati ya watunga sera, jamii za wenyeji, na wanahifadhi ili kuunda sera za matumizi ya ardhi zinazozingatia usawa.

Profesa Shivji anapendekeza kuwa majadiliano hayo yawe ya uwazi na yenye ushirikishwaji.

Related Posts