Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeshiriki mkutano wa Baraza la Shirikisho la Wahasibu Duniani (IFAC Council 2024) unaofanyika jijini Paris nchini Ufaransa kuanzia tarehe 6 hadi 7 Novemba, 2024 ambapo kwenye mkutano huo mambo mbalimbali yamejadiliwa ili kuendeleza taaluma ya Uhasibu duniani.
Katika mkutano huo Tanzania kupitia NBAA iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania , CPA. Prof. Sylvia S.Temu na Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA CPA Pius Maneno.
Katika mkutano huo, Rais na Naibu Rais wapya wa IFAC wamechaguliwa kwa kipindi cha 2025 -2027 ambao ni Bw. Jean Bouquot kutoka Ufaransa na Bi. Taryn Rulton kutoka Australia.
Ikumbukwe kwamba Shirikisho la Wahasibu Duniani (IFAC) kupitia Ripoti yake ‘International Public Sector Financial Accountability Index -2021 Status- 2020 Index Financial Reporting Bases’ iliitangaza Tanzania na Nigeria kushika nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika katika utumiaji wa viwango vya kimataifa vya Utayarishaji wa Taarifa za Fedha za Umma (IPSAS).
Sambamba na hilo Tanzania imeendelea kung’ara kimataifa kwani kupitia NBAA, mtanzania CPA Dkt Neema Kiure alichagulia kuwa mjumbe wa Kamati ya Uteuzi ‘Nomination Committee’ ya IFAC kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwezi Januari 2024. Vile vile mtanzania CPA Simon Mponji amechaguliwa kuwa mjumbe wa “Accountancy Quality Advisory Group” la Shirikisho la Wahasibu la Afrika (PAFA) kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2025 hadi 2027.
Mkutano wa Shirikisho la Wahasibu Duniani (IFAC Council 2024) uliofanyika jijini Paris nchini Ufaransa kuanzia tarehe 6 hadi 7 Novemba, 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Pius Maneno (wa kwanza kulia) akiwa na baadhi ya washiriki wa mkutano wa IFAC kutoka kushoto ni Rais wa ICPAK -Kenya CPA Philip Kakai, Mkurugenzi Mtendaji wa IFAC Lee White, Mkurugenzi Mtendaji wa ICPAU-Uganda CPA Derick Nkajja, Rais wa IFAC Bibi Asmâa Resmouki (2023-24) na Rais wa OPC Burundi, Frederick Gahungu.