WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa nchini waakisi utashi wa kisiasa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia na kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.
“’Utashi wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mfumo wa utoaji wa Haki Jinai lazima udhihirike kwenu ninyi viongozi mlio karibu na wananchi. Hata hivyo, utashi huo hauwezi kudhihirika kwenu iwapo hamtakuwa na nia ya dhati ya kubadilika na kisha kuongoza mabadiliko kwenye maeneo mnayomwakilisha Mheshimiwa Rais wetu na hususan katika kuhudumia wananchi,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Mei 6, 2024) wakati akifungua warsha ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya kuwajengea uelewa kuhusu maboresho kwenye mfumo wa Haki Jinai na utoaji wa haki nchini kwenye ukumbi wa mikutano wa Tume Huru ya Uchaguzi, uliopo Njedengwa, nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
Amesema sambamba na suala la utashi, ni lazima viongozi na watendaji wa Serikali wawe na uelewa wa kutosha ili waweze kuyasimamia na kuyatekeleza mapendekezo hayo.
Amesema malalamiko ya wananchi katika masuala kadhaa ndiyo yaliyoweka msukumo kwa Mheshimiwa Rais kuunda Tume ya Haki Jinai na kuyakubali mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo na hatimaye kuigeuza kuwa Kamati ya kuandaa mikakati utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.
“Hivyo basi, kwa kuwa ninyi ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais katika maeneo yenu ya utawala, ni wajibu wenu kuhakikisha kuwa azma ya Mheshimiwa Rais inatimia kwa kusimamia na kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai,” amesisitiza.
Akitaja masuala yaliyolalamikiwa na wananchi, Waziri Mkuu amesema utungaji wa baadhi ya sheria ndogo katika mamlaka zao ambazo aghalabu hukinzana na sheria mama. “Mfano ni tozo zinazoanzishwa na halmashauri kama vile ushuru wa mabango, kodi za maegesho na usimamizi wa matumizi ya maeneo ya barabara zinasababisha mkanganyiko kwa wananchi kwa kuwajibishwa na chombo zaidi ya kimoja,” amesema.
Masuala mengine ni migogoro ya ardhi, matumizi mabaya ya madaraka ya ukamataji na desturi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuambatana na Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama katika ziara mbalimbali hata zile zisizohitaji uwepo wa vyombo hivyo, hali ambayo imekuwa ikisababisha hofu kwa wananchi na kuwafanya washindwe kufikisha mawazo na kero zao kwa viongozi hao.
Amewataka viongozi wote walioshiriki warsha hiyo wazingatie maelezo yatakayotolewa ili kila mmoja akawe chachu ya mabadiliko ya kifikra, kimtizamo na kiutendaji katika eneo lake. “Wakuu wa Mikoa na viongozi wote mlioshiriki katika warsha hii, endeleeni kushirikiana na taasisi za Haki Jinai katika utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya kuboresha mfumo na utendaji wa taasisi hizi.”
Amewataka wazingatie uwepo wa majengo na miundombinu muhimu kwa ajili ya taasisi za Haki Jinai katika maeneo mapya ya utawala (Wilaya) yaliyoanzishwa. “Kuna maeneo mengi mapya ya utawala bado huduma za Haki Jinai kama vile vituo vya Polisi na magereza hazijafika na wananchi wanapata taabu sana kuzifikia huduma hizo katika Wilaya mama ikiwemo kutembea au kusafiri kwa muda mrefu,” amesisitiza.
Mapema, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange alisema kuwa ofisi hiyo itasimamia utekelezaji wa maagizo na maelekezo yatakayotolewa katika warsha hiyo ili dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona wananchi wanapata haki zao inafikiwa.
“Naomba nitumie nafasi hii kukuhakikishia kuwa yote ambayo tutajifunza katika warsha hii na maelekezo yote ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu utatupa tutahakikisha tunakwenda kuyatekeleza katika mikoa na halmashauri zetu ili dhamira ya mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yaweze kufikiwa.”
Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande alisema Kamati yao iliundwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Septemba 2023 ili kufanyia kazi ripoti ya Tume iliyokuwa na mapendekezo 333 ya maboresho ya utendaji kazi wa taasisi za haki jinai katika maeneo mbalimbali.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa matukio ya uhalifu nchini yanazidi kuongeza mwaka hadi mwaka na kwamba juhudi kubwa zinaelekezwa kupambana na uhalifu badala ya kubaini na kuuzuia.
“Moja ya majukumu tuliyopewa kwenye kamati hii ni kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kubaini na Kuzuia Uhalifu unaotarajiwa kuwa nyenzo ya utekelezaji wa taasisi na mamlaka zote zinazohusika ili kukabiliana na janga la uhalifu nchini,” alisema na kuongeza kuwa viongozi na watendaji wote watakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa mkakati huo utakaporidhiwa na Serikali ili malengo yake yaweze kutimia.