DAWASA NA TANESCO WAKUBALIANA KUIMARISHA HUDUMA DAR NA PWANI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amezitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kudumisha ushirikiano baina yao ili kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi.

Mhandisi Waziri amesema kuwa Taasisi hizi ni za Serikali na zinafanya kazi moja ya kuhudumia wananchi kwenye sekta ya Majisafi na Nishati, hivyo ni vyema zikashirikiana ili kuleta ufanisi kwa Serikali.

Amesema kuwa TANESCO inapaswa kuisaidia DAWASA hususani kwenye kuhakikisha umeme unaotumika kuendesha mitambo ya uzalishaji maji unakuwa wa uhakika muda wote ili kutoathiri utoaji wa huduma kwa wateja.

“Serikali imetuamini kufanya kazi ya kutoa huduma bora kwa Wananchi, hivyo tunapaswa kuwa kitu kimoja kwenye uendeshaji wa shughuli zetu za kila siku, na jitihada hizi zitasaidia kuongeza ufanisi kwenye utoaji wa huduma,” alisisitiza Mhandisi Waziri.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa kikao cha Taasisi hizi ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali yanayozitaka Taasisi hizi ziweze kuimarisha Mawasiliano kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wateja wote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TANESCO Kanda ya Mashariki, Mhandisi Kenneth Boymanda amesema kuwa ushirikiano baina ya Taasisi hizi ni wa muhimu sana na utasaidia kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwenye maeneo ya vyanzo vya maji ikiwemo Mitamboni ili wananchi wapate maji bila kuwa na changamoto zozote.


Related Posts