Lema aamuru maofisa Takukuru kutoka ukumbini semina ya wagombea wa Chadema

Arusha. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amewafukuza ukumbini maofisa watatu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwenye semina ya wagombea wa serikali za mitaa.

Tukio hilo limetokea leo Alhamisi, Novemba 7, 2024 katika Hoteli ya Golden Rose ambapo Chadema Mkoa wa Arusha imefanya semina kwa wagombea uenyekiti na ujumbe wa uchaguzi huo.

Lengo la kuwapatia wagombea wao wa uenyekiti na ujumbe wa serikali za mitaa utaratibu wa kufanya kampeni kwa wananchi kuelekea uchaguzi wao utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Katika semina hiyo Lema aliyekuwa mgeni rasmi ambaye aliingia ukumbini saa tisa alasiri na kukuta taratibu zingine zikiendelea za kuwajulisha wagombea tarehe ya kuanza kampeni ni Novemba 20, 2024 hivyo wawe tayari.

Lema baada ya kuingia na kupata utambulisho ikiwemo maofisa hao wa Takukuru, alisimama na kusema hakubaliani na maofisa hao kuzungumza na wajumbe wao wanaogombea nafasi za uongozi.

“Sitakubali muongee na wajumbe wetu wakati mmeshindwa kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa serikali wakiwemo wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao.

Pia, waandikishaji wa daftari la wapiga kura kwa vitendo walivyokuwa wanafanya hivyo naombeni muondoke hatuwahitaji hapa, tungekaa kuwasikiliza endapo mngeanza kudhibiti vitendo hivi,” amedai Lema.

Hata hivyo, maofisa hao waliokuwa wamekaa meza za mbele kwa wageni rasmi hawakunyanyuka hadi wasimamizi wa ulinzi wa semina hiyo walivyowafuata na kuwanyanyua kwa nguvu ndipo wakaamua kutoka huku wakizomewa na wajumbe wa semina hiyo.

Awali, mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha Mjini, Elisa Mungure amesema wakati wakiandaa mkutano huo, walikuja maofisa hao na kujitambulisha wanatoka Ofisi ya Takukuru wanaomba kutoa semina ya vitendo vya rushwa kuelekea kampeni na uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Sisi hatukuweza kuwakatalia hivyo tuliwakaribisha na wakaa mbele kabla ya kumpigia mwenyekiti wetu ambae ndio mgeni wetu rasmi kumjulisha na kusema anakuja, na kweli akaja,” amesema Mungure.

Mwananchi limemtafuta kwa simu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo kuhusu tukio hilo ambapo amesema swala hilo si jema lakini haiwezi kuzuia elimu ya rushwa kuwafikia wananchi.

“Wao wamezuia leo lakini haiwezi kuathiri chochote kwani tutatoa elimu hata sehemu nyingine kwa wakati mwingine kupitia njia nyingine hata kwenye vyombo vya habari na mikutano ya kidini, kisiasa na kwenye sehemu ya hadhara ila sio jambo jema lililofanyika,” amesema Zawadi.

Related Posts