Kina cha migodi, mabadiliko ya teknolojia changamoto sekta ya madini

Dar es Salaam. Uhaba wa wataalamu wa kuendesha mitambo mikubwa ya migodini imetajwa kuwa changamoto inayoikabili sekta ya uchimbaji madini kwa sasa nchini.

Hali hiyo inatokana na kina cha migodi kwenda chini ya ardhi suala linalolazimu kukodi wataalamu kutoka nje kuendesha mitambo hiyo mikubwa ya chini ya ardhi ikiwemo mitambo ya Jumbo.

Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Wachimbaji Wakubwa na Kati linalojulikana pia Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi, Benjamin Mchwampaka amesema hayo leo Novemba 7, 2024 akichangia mjadala wa Mwananchi X Space ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano na Wizara ya Madini na Chemba ya Migodi Tanzania kujadili mada isemayo ‘Tulipo, tunapokwenda, kuelekea mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania’.

Mchwampaka amesema mtaalamu mmoja akikodiwa kuendesha Jumbo analipwa gharama kubwa kwa mwezi kama mshahara na marupurupu mengine.

Amesema kutokana na hilo Chemba ya Migodi imechukua hatua ya kuwasaidia Watanzania kupata ujuzi utakaosaidia kufanya kazi hizo na kuacha kupeleka fedha nje.

“Sisi kama Chemba tumeona hapana, tumeandaa mitalaa sita kwa ajili ya kufundisha Watanzania. Tunashauri Serikali itupie jicho programu kama hii kuongezea nguvu. Tunatamani juhudi tunazofanya ziungwe mkono,” amesema.

Amesema uhitaji wa watalaamu unakua mkubwa kadri siku zinavyokwenda kutokana na fursa zilizopo kwenye sekta ya madini.

Ameshauri kuwa ipo haja ya Serikali na sekta binafsi kukaa mezani kwa pamoja kutatua changamoto zinazoikumba sekta hiyo kwa lengo la kuendelea kuikuza.

Mchwampaka amesema Chemba imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali, ikiwemo kuwapeleka Watanzania kwenda kusoma nje ya nchi ili kupata ujuzi kuhakikisha wanashiriki kwenye mnyororo wa thamani na kuacha kupeleka fedha nyingi kwa wageni.

“Tunatoa mafunzo kwa vitendo kwa wataalamu wa Kitanzania na tunajivunia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuacha kupeleka fedha zetu nje,” amesema.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Chuo cha Madini, Elvanus Kapira amesema wajibu wao ni kuzalisha wataalamu watakaoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia yaliyopo hivi sasa.

Kapira amesema usipokuwapo umakini inawezekana kuzalishwa wataalamu wenye ujuzi wa teknolojia za zamani.

“Teknolojia za sasa ni mpya na watu wanaowafundisha wataalamu wa sekta ya madini hawakuwafundisha teknolijia mpya. Changamoto zilizopo katika sekta ikiwemo ya elimu inachochochewa na mabadiliko ya teknolojia,” amesema.

Amesema wana mpango wa kushirikiana na sekta binafsi, ambao wataeleza mahitaji yao na kuainisha shida iko wapi ili wasaidiane katika maeneo hayo kwa kuanza na tafiti.

“Mfano anaongelea mashine za migodini hizo za kisasa na sisi kama chuo hatuna fedha, watuunganishe na hao wenye nazo tuwapeleke wanafunzi wazawa wakajifunze,” amesema na kuongeza:

“Kazi yetu ni kuhakikisha wizara inaenda na muda kutokana na teknolojia zinavyobadilika kila wakati,” amesema.

Katika hoja hiyo, mtaalamu wa Uchumi, Oscar Mkude amesema kuna haja ya kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani hasa katika madini ya kimkakati ili kuwapa urahisi wanapokutana na wawekezaji.

Mkude amesema jambo hilo litawafanya wawe makini, wafanye kazi kwa weledi na kasi kubwa.

“Wawekezaji wakati mwingine hawana shida kuwekeza ila uamuzi unachukua muda mrefu kiasi cha kuwatia mashaka kuwa kama hakukuwa na utayari wa kutaka uwekezaji huo ufanyike, hivyo ni vyema wataalamu wajengewe uwezo wa kukabiliana na wenzao,” amesema.

Mbali ya hilo, amesema ni vyema kuangalia namna sekta ya madini inavyosimamiwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutengeneza mazingira ya rushwa.

Amesema hilo litawezekana kwa kuondoa mazingira yote yanayofanya watu waone mambo yanafanyika ndivyo sivyo au kwa njia za mkato.

“Ni vyena kuangalia usimamizi wa sekta yetu ya madini ukoje ili kile kinachopatikana kiwe stahiki kwa nchi yetu na hakuna mtu anayeweza kukitumia kwa namna nyingine,” amesema.

Amesema jitihada zinazofanywa ni kwa ajili ya Watanzania na si watu wachache.

“Kufanya hivi kutasaidia kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye nchi na maisha ya Mtanzania mmoja mmoja,” amesema.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali inatarajia kujenga maabara kubwa ya kisasa ya madini jijini Dodoma kupima sampuli za madini nchini.

Amesema hatua hiyo itasaidia wachimbaji wanaokwenda kwenye maabara binafsi na hata nje ya nchi kupima sampuli hizo.

Amesema ukamilishwaji wa maabara hiyo utakuwa chachu katika ukuaji wa sekta ya madini ambayo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi.

Waziri amesema maabara pia itajengwa Geita na Mkoa wa Madini Chunya. Amesema yote hayo yametokana na ongezeko la bajeti ya sekta hiyo.

Mavunde amesema sekta hiyo imeendelea kukua mwaka hadi mwaka tofauti na kipindi cha miaka mitano hadi sita iliyopita.

Ukuaji huo amesema unatokana na kufanyika marekebisho makubwa ya sheria ya mwaka 2017 ambayo yameleta mageuzi yanayoifanya sekta ya madini kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Mwaka 2022 mchango wa sekta hii kwenye pato la Taifa ilikuwa asilimia 7.2. Mwaka 2023 ikawa asilimia 9.0 ila malengo tuliyojiwekea ifikie asilimia 10 mwaka 2025,” amesema.

Katibu Mkuu, Wizara ya Madini, Yahaya Samamba amesema Serikali ina mkakati wa kuja na programu ya Jenga Kesho iliyo Bora kupitia madini (MBT).

Katika utekelezaji wa programu hiyo, amesema baadhi ya sehemu za leseni za maeno ya kuchimba madini zitakabidhiwa kwa vijana waweze kujikimu kutokana na changamoto ya ajira iliyopo hivi sasa.

“Hilo linafanyika baada ya kutengwa kwa maeneo na kufanyiwa utafiti na mikopo inapatikana,” amesema.

Amesema tayari benki zaidi ya 10 zimeridhia kutoa mikopo ili watu waweze kuendeleza maeneo waliyonayo na yale watakayogawiwa.

Amesema hilo linafanyika kwa sababu Serikali inatambua kuwa wawekezaji wa ndani wakilelewa vizuri kunakuwa na uhakika wa ajira na mapato yanayopatikana yanaweza kutumika ndani ya nchi kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Mnakuwa na uhakika kuwa fedha zitatumika ndani, zitanunua bidhaa za ndani zitaajiri watu wa ndani na kuwekeza ndani,” amesema.

Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Madini Tanzania, Mhandisi Ramadhan Lwano amesema uchimbaji wa madini ukifanyika bila kujali mazingira faida yake ni ndogo.

Hilo ni kwa sababu mgodi ukimaliza kufanya shughuli zake, fedha nyingi zitatumika kukarabati mazingira na faida ya mgodi huo haitaonekana.

Lwano amesema mikakati ya Serikali ni kuhakikisha wachimbaji wanaelekezwa nini cha kufanya, huku wanaokiuka hupewa adhabu na kuamriwa kurekebisha taratibu za uchimbaji ili kuendana na mazingira salama.

“Mazingira yakiwa salama kwa hali ya juu shughuli za uzalishaji madini zinapokwisha mgodi unafungwa na kuwekwa chini ya uangalizi ili kuangalia athari za mazingira na namna jamii inavyoweza kuishi eneo hilo hata shughuli za uchimaji zinapokamilika,” amesema.

Amesema Tume ya Madini inaendelea kusimamia hilo kwa kutoa elimu na usimamizi wa karibu ili kuhakikisha shughuli za madini zinakuwa na faida kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Related Posts