Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Vijana 1,000 walio mtaani ambao hawasomi wanatarajia kunufaika kiuchumi kwa kupata stadi za maisha, elimu ya kusimamia biashara na ujasiriamali, kukuza mitaji na kutumia majukwaa ya kidijitali kukuza biashara zao kupitia mradi wa Vijana Elimu Malezi na ajira (VEMA) unaolenga kuwawezesha kiuchumi.
Hayo yamebainishwa jijini hapa katika kikao cha kujadili mrejesho wa utekelezaji wa mradi huo wa miaka miwili (2022-2026) unatekelezwa na mashirika ya SEDIT, VETA na Plan International kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji katika kata 13 za wilaya ya Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza ukiwalenga vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24.
Afisa Miradi Shirika la SEDIT, Nahumu Fungo amesema mradi huo umelenga kuwapatia ustadi na utaalam mbalimbali vijana walioko nje ya kwa kuwaunganisha kwenye vikundi, kuwajengea uwezo na kupata fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kufundishwa kuweka akiba na kutunisha kipato chao ili waweze kukopesha, kusimamia biashara na stadi za maisha ili wapate utaalam na kujiajiri.
Amesema tangu kuanza kwa mradi huo vikundi 49 (30 Ilemela na 19 Nyamagana) vimeundwa huku lengo likiwa ni kuunda vikundi 50 vyenye angalau wanachama 30 na kuwafikia vijana 1,000 (asilimia 60 wasichana, 40 wavulana na asilimia 5 wenye ulemavu). Mpaka sasa wamewafikia vijana 886 (wasichana 453 na wavulana 433) wakiwemo 446 kutoka Ilemela na 440 Nyamagana huku wakiwa na upungufu wa vijana 114 kwenye vikundi.
“Tumeshahamasisha vikundi kufungua akaunti kwenye benki ili kuviwezesha kupata mikopo na tayari vikundi 11 vimefanya hivyo, vijana 320 wameanzisha biashara zao ndogo baada ya kujengewa uwezo na wengine 328 waliokuwa na biashara zao wameziboresha kutokana na utaratibu wa kukopesha kwenye vikundi,” amesema Fungo
Hat hivyo, Fungo ameeleza kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto ya vijana kujitoa kwenye vikundi kwa baadhi yao kukosa uvumilivu, kuhama maeneo na wazazi kuwakataza, huku wakikabiliwa pia na changamoto ya urasimu katika mifumo ya kusajili vikundi hivyo katika halmashauri kutokana ucheleweshaji.
Marry Robert, mkazi wa Buswelu wilayani Ilemela aliyenufaika kupitia mradi huo kwa kuanzisha biashara ya genge la mbogamboga kwa mtaji wa Sh 50,000 Juni, mwaka huu, amesema amejifunza kutunza fedha, kukopa na kuanzisha biashara huku akiwa na malengo ya kukuza biashara hiyo kwa mbinu alizofundishwa na kuifanya iwe kubwa.
Naye, Abel Samson, mkazi wa Kayenze Ilemela amesema “Mradi ulinikuta najishughulisha na kuuza dagaa umeniongezea maarifa ya biashara, kuongeza mtaji, kuweka akiba, kupata mkopo na kuongeza masoko. Nawashauri vijana wawe na imani na msimamo wanapoletewa miradi ili wapate ujuzi na kunufaika badala ya kukengeuka na kukata tamaa mapema,”
Mratibu wa mradi wa Vema kutoka shirika la Plan International, Gadiel Kayanda amesema pamoja na kuwawezesha vijana kiuchumi mradi huo pia unatekelezwa katika maeneo ya elimu jumuishi, kulinda watoto dhidi ya ukatili, na kuboresha mazingira ya kujifunzia shuleni, huku zaidi ya Sh milioni 100 zikiwekwa na vijana kupitia vikundi vyao tangu mradi huo uanze, ambapo fedha hizo zimewasaidia kukopesha na kuanzisha miradi mbalimbali.
Afisa Maendeleo Mwandamizi halmashauri ya jiji la Mwanza, Moshi Masinde ameshauri taasisi zinazotekeleza miradi ya kusaidia jamii kukaa pamoja kupitia majukwaa yao ili kama miradi inafanana watekeleze kwa pamoja ama wagawane maeneo ili kusaidia kupunguza mgongano wa miradi katika eneo moja jambo ambalo linafanya matokeo yaliyokusudiwa yasifikiwe.
“Serikali pia isaidie kwa kuainisha maeneo yenye mahitaji kuyasaidia mashirika kuwafikia walengwa kuliko kurundikana sehemu moja isiyo na uhitaji. Kabla hatujatekeleza mradi eneo fulani ni vyema kulitembelea eneo husika ukaona kwa macho na kusikia mwenyewe hii inakusaidia kuwa na ufahamu na kutekeleza mradi wako kwa mafanikio,” amesema Masinde.
Naye, Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Mwanza, Rehema Mkwize amesema hoja za wadau zilizowasilishwa kuhusu changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya aina hiyo zitafanyiwa kazi, huku akiyataka mashirika yanayotekeleza miradi mkoani Mwanza kuwa tayari kunyumbulika na kufanya kazi katika maeneo yasiyopewa kipaumbele mara kwa mara.
“Ni vyema sasa mashirika yanapoandika miradi yawatumie na kuwashirikisha maafisa kwenye maeneo husika ili kupata taarifa sahihi, na kwa upande wa maafisa wa Serikali mdau anapokuja aambiwe eneo Fulani kuna watu wengine ili aende ama ahamishiwe eneo linguine. Kwahiyo tukubaliane kunyumbulika na sisi tunakwenda kuyafanyia kazi hoja zilizowasilishwa hapa,” amesema Mkwize.