Dodoma. Wakati Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina akirejea bungeni na kuonyesha uwepo wake, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amembananisha kuhusu kauli yake kuwa Kampuni ya DP World inatoza kodi.
Leo Alhamisi Novemba 7, 2024, Mpina amerejea bungeni baada ya adhabu aliyopewa ya kutohudhuria vikao 15 vya Bunge kumalizika katika mkutano wa Bunge wa bajeti uliopita.
Katika Bunge la Bajeti Juni 2024 pamoja na mambo mengine Mpina alidai kampuni zilizopewa vibali vya kuagiza sukari hazikuingiza sukari nchini na kwamba Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alikataa kufanya kikao na wadau wa sukari.
Hatua hiyo ilimfanya, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimpeleka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za kulidharau Bunge na Mamlaka ya Spika na kumtaka kuwasilisha ushahidi wake kuwa Waziri Bashe alilidanganya Bunge kuhusu suala la upungufu wa sukari.
Hata hivyo, Juni 24, 2024, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Ally Makoa alilieleza Bunge kuwa limemkuta na hatia ya kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge na kupendekeza adhabu hiyo ya kusimamishwa vikao 15 ambapo Bunge liliiridhia.
Pamoja na kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu leo Alhamisi, Mpina amepata nafasi ya kuwasilisha mchango wake katika hoja mbili zilizokuwa zikijadiliwa katika Kamati ya Bunge zima.
Hoja zilizokuwa zikijadiliwa na kutolewa ushauri ni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2025/26 na Mwongozo wa Mapendekezo ya Bajeti kwa mwaka 2025/26.
Akichangia mjadala huo, Mpina amesema DP World ilisema itawekeza Dola milioni 250 sawa na Sh687 bilioni kwa miaka mitano lakini mwekezaji huyo anakusanya kodi sasa.
Amesema lakini alisema walikubaliana mikataba mitatu ya nchi mwenyeji (HGA) yote ipelekwe katika Bunge ili kuona ni nini ambacho kilikubalika ndani ya mikataba hiyo.
“Lakini Sheria ya Rasilimali za Maliasili inasema mikataba yote ya rasilimali lazima iletwe hapa bungeni. Naendelea kuuliza hivi imeshindikana nini kuleta mikataba ya Bandari ya Dar es Salaam tuliyoingia mkataba na DP World hapa bungeni,” amehoji.
Amehoji ni nani alienda kukubali uwekezaji wa DP World wa Sh687 bilioni na nani aliyeenda mapato yanayotokana na shughuli za bandari hiyo ni asilimia 40 kwa 60.
Ameomba mikataba hiyo kupelekwa bungeni ili waweweze kuona kilichomo ndani yake.
Baada ya Bunge kurejea, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliomba kuhusu utaratibu ambapo amesema Mpina katika mchango wake ameliambia Bunge kuwa DP World imeanza kukusanya kodi.
Amesema yeye ndiye Waziri wa Fedha na kuwa mamlaka inayokusanya kodi ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iko chini yake.
“Nalidhibitishia Bunge hakuna kodi yoyote inayoruhusiwa kukusanywa na taasisi yoyote isiyo ya Serikali au ambayo haijapewa jukumu hilo,” amesema Dk Mwigulu.
“Kwa hiyo kodi hiyo ya DP World aliyokuwa anaiongelea hakuna kodi yoyote ambayo DP World inakusanywa bandarini zote zinakusanywa na TRA. Na kimsingi baada ya DP World kuanza shughuli zile ambazo zimeongeza kodi, kodi inayokusanywa TRA imeongezeka na kugota Sh1.23 trilioni,”amesema.
Amesema kiwango hicho hakijawahi kufikiwa na tangu kauli ya Mpina kuwa DP World imeanza kukusanya kodi ni ya uongo na imelenga kupotesha Bunge na Watanzania na kama hajafanya kwa makusudi aifute.
Baada ya kueleza hayo, Naibu Spika wa Bunge, Musa Zungu alimpa nafasi Mpina kufuta kauli yake ama kuleta udhibitisho kuhusu kampuni hiyo kuanza kutoza kodi katika bandari hiyo.
Akizungumza baada ya kutakiwa kufanya hivyo, Mpina amesema kama katika mchango wake alitumia neno kodi alimaanisha tozo zinazokusanywa na DP World baada ya kuwa imekabidhiwa tangu Aprili 24, 2024.
Amesema amelitumia neno kodi kukusanywa na alifuta neno hilo katika kumbukumbu rasmi za Bunge na kuwa yeye alimaanisha tozo zinatoza kampuni hiyo.
Zungu alimpongeza Dk Mwigulu kwa kuweza kuchambua na kubaini vitu hivyo ambavyo vinapeleka taswira mbaya na taarifa za uongo kwa wananchi ambazo siyo za kweli.
“Na mheshimiwa Mpina umefuta kauli yako naomba sasa katibu aliyoko mezani na kumbukumbu rasmi za Bunge taarifa ya kuwa DP World inakusanya kodi iondolewe katika kumbukumbu zetu za Bunge,” amesema.
Amesema wanataka mawaziri kama Dk Mwigulu wakiona jambo ambalo linaleta ukakasi unasimama na kulisemea ukweli.
Kishimba awashushia lawama HESLB, vyuo
Akichangia mjadala bungeni, Mbunge wa Kahama (CCM), Jumanne Kishimba amesema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ilivipatia vyuo fedha ambazo walitoa elimu kwa wanafunzi.
“Chuo kimempa elimu mwanafunzi elimu ambayo haiajiriki anayetakiwa kushtakiwa kabisa ni nani (kwa kutorejesha mikopo) ni mwanafunzi ama ni chuo. Kwa sababu dunia inabadilika hatuwezi kuendelea na dunia ile ile kuwa elimu ni ufunguo wa maisha hapana,” amesema.
Amesema elimu ni bidhaa na kuwa wahitimu walishindwa kurejesha kwa kuwa wameshindwa kuuza, hivyo wanaotakiwa kushtakiwa kwa kushindwa kuirejesha mikopo ni HESLB.
“Kwanini tusiweke kuwa chuo chochote kinachotaka kuingia katika mfumo wa mikopo kwa kupewa na HESLB, kikidhi kigezo cha kuwa na mtalaa unaouzika,” amesema.
Ametoa mfano kama mwaka jana walimaliza wanafunzi 300 basi asilimia 70 wawe wamepata ajira ndipo kikidhi takwa la kupewa mkopo na HESLB.
Amesema vyuo kutoa daraja la ufaulu (GPA) ambazo haziajiriki kutaifanya bodi hiyo kufilisika kwa kuwa wahitimu wasipopata ajira hawawezi kulipa mikopo wanayopewa na bodi hiyo.