BAADA ya kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili kutokana na kuvunjika kidole, winga wa Singida Black Stars, Edmund John amerejea na yuko fiti kukiwasha kikosini na sasa amempa kibarua kocha Patrick Aussems cha kupanga kikosi kutokana na ushindani uliopo kwenye timu hiyo.
Winga huyo aliyejiunga na Singida msimu huu akitokea Geita Gold iliyoshuka daraja, hajacheza mchezo wowote wa ligi tangu alipotua kutokana na kikosi hicho kusheheni mastaa mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na Mwanaspoti Edmund, alilisema kwa sasa amepona na amekuwa anafanya mazoezi binafsi na ameimarika na timu ya madaktari imemruhusu kuanza kujifua na wenzake huku akiamini muda mwafaka ukifika benchi la ufundi litampa nafasi na kuisaidia timu hiyo.
“Mapambano ya namba yanaendelea ila kabla ya ligi kuanza nilipata majeraha, sasa ndio nimerejea tena kwenye kikosi kwahiyo tunazidi kupambana. Mfupa wa kidole ulimeguka nimekaa nje karibu miezi miwili, lakini sasa nimeanza mazoezi na timu,” alisema Edmund ambaye kwa misimu miwili iliyopita alifunga mabao matano ya Ligi, likiwamo moja wakati Geita ikishuka daraja.
“Hii si mara yangu ya kwanza, wachezaji wenye uzoefu mkubwa nimeshakaa nao wengi kwahiyo huu utakuwa mwendelezo na kufanikisha ninachohitaji kufanya kwa kujifunza na kuboresha kipaji changu,” alisema.
Alisema malengo yao ni kumaliza ndani ya nafasi mbili za juu mwishoni mwa msimu huku akitamba huduma nzuri wanayopewa na menejimenti pamoja na ubora wa wachezaji waliopo ni sababu zitakazowasaidia kutimiza malengo hayo.