Matumizi ya teknolojia katika kilimo yametajwa kuwa na mchango chanya katika kukuza na kukifanya kilimo kuwa na tija kwa wakulima.
Hayo yamejiri Mjini Morogoro kwenye mkutano wa 16 wa kisayansi wa Chama cha Wachumi Kilimo Tanzania (AGREST) wakati wakijadili matokeo ya tafiti mbalimbali ya ambazo wamezifanya, wakijikita katika kilimo digitali ambacho kinampa nafasi mkulima kutumia teknolojia kuongeza tija katika kilimo
Mwenyekiti wa AGREST, Dkt. Florens Turuka amesema kama ambavyo teknolojia inatumika katika nyanja nyingine ni wakati wa sekta ya kilimo kuboreshwa kwa matumizi ya kidigitali ikiwemo katika kutumia akili mnemba, roboti na ndege isiyokuwa na rubani ili kubaini changamoto za mazao shambani, kubaini aina ya udongo na mbolea gani itumike.
“Saizi mkulima hatakiwi kubahatisha kuhusu mbolea ya kutumia na hata kuuza mazao yake anaweza akabakia nyumbani akapata bei kwa njia ya kidigitali suala ambalo linampunguzia usumbufu na kufanya shughuli za kilimo kuwa rahisi tofauti na ilivyokuwa awali”, alisema Dkt. Turuka.
Amesema kupitia kikao hicho, wanakusudia watatoka na mapendekezo mbalimbali ya kuishauri serikali ili ikione yanafaa waweze kuyaingiza kwenye sera zake.